Wanajeshi wa Congo Brazzaville watishiwa kufukuzwa CAR
Kamanda wa kikosi cha Umoja wa Mataifa kinacholinda amani Jamhuri ya Afrika ya Kati ametishia kuwafukuza wanajeshi wa Congo Brazzaville wanaolinda amani nchini humo kutokana na utovu wa nidhamu.
Shirika la habari la AFP limeripoti kuwa, kwa mujibu wa hati ya siri iliyosambazwa jana Jumanne, Jenerali Bala Keita, kamanda wa kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani Jamhuri ya Afrika ya Kati (MINUSCA) ametishia kuwafukuza wanajeshi wa Congo Brazzaville kutokana na kuwanyanyasa watu kijinsia na kutokuwa na nidhamu jeshini.
Amesema, Congo Brazzaville inapaswa ichukue hatua za haraka za kufikia viwango vya nidhamu jeshini kwa mujibu wa kikosi cha MINUSCA vinginevyo kutachukuliwa hatua ya kuwafukuza wanajeshi wa nchi hiyo Jamhuri ya Afrika ya Kati na kupelekwa wanajeshi wa nchi nyingine.
Wakati huo huo msemaji wa kikosi hicho cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa amesema, vitendo vya askari wa Congo Brazzaville huko Jamhuri ya Afrika ya Kati vinapimwa kwa mujibu wa vigezo vya kikosi cha MINUSCA na inabidi askari hao wa Congo Brazzavile wafanye juhudi za kufikia viwango hivyo kwani utovu wowote wa nidhamu hauwezi kusamehewa.
Wanajeshi wa kofia buluu wa Congo Brazzaville walitumwa katika mji wa Bambari wa katikati mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati tarehe 17 Septemba 2016.
Itakumbukwa kuwa tangu mwaka 2013, Jamhuri ya Afrika ya Kati ambayo inahesabiwa kuwa moja ya nchi maskini zaidi duniani, inashuhudia machafuko na mapigano ya makundi yenye silaha kiasi kwamba, askari wa Umoja wa Mataifa wametumwa nchini humo kwa ajili ya kulinda amani.