Maelfu ya raia wa CAR wakimbilia mkoa wa Equator Kongo DR
Habari kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zinaarifu kuwa, tangu mwezi Mei mwaka huu, hadi hivi sasa zaidi ya wakimbizi elfu 30 kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati, wameingia katika mkoa wa Equator wa kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.
Taarifa iliyotolewa na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) imesema kuwa, hadi sasa maelfu ya wakimbizi kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati wapo katika mkoa huo. Shirika hilo limeongeza kuwa, raia hao wa CAR wamelazimika kuyakimbia makazi yao kwenda ughaibuni kutokana na mashambulizi ya makundi ya Anti-Balaka na Seleka ambayo yamekuwa yakiendesha hujuma za ulipizaji kisasi kati yao.
Hii ni katika hali ambayo, licha ya Umoja wa Mataifa kuahidi kutoa misaada kwa ajili ya wakimbizi hao, lakini hadi sasa bado wanaishi katika mazingira magumu kutokana na kukosa misaada hiyo. Jamhuri ya Afrika ya Kati ilitumbukia katika mchafuko mwaka 2013, baada ya waasi wa Seleka kumpindua aliyekuwa rais wa nchi hiyo, François Bozizé. Baada ya tukio hilo kundi la Kikristo lenye misimamo ya kuchupa mipaka la Anti-Balaka lilianzisha mauaji ya halaiki dhidi ya Waislamu wasio na hatia na kuua maelfu ya watu wa jamii hiyo.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, Jamhuri ya Afrika ya Kati kuna maelfu ya askari wa Umoja wa Mataifa wanaosimamia amani.