Magaidi watatu wauawa katika Rasi ya Sinai, kaskazini mwa Misri
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i30568-magaidi_watatu_wauawa_katika_rasi_ya_sinai_kaskazini_mwa_misri
Msemaji wa jeshi la Misri amesema kuwa, jeshi la nchi hiyo limefanikiwa kuua magaidi watatu katika Rasi ya Sinai, kaskazini mwa nchi hiyo.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Jun 16, 2017 23:03 UTC
  • Magaidi watatu wauawa katika Rasi ya Sinai, kaskazini mwa Misri

Msemaji wa jeshi la Misri amesema kuwa, jeshi la nchi hiyo limefanikiwa kuua magaidi watatu katika Rasi ya Sinai, kaskazini mwa nchi hiyo.

Tamir al Refai alisema hayo jana (Ijumaa) na kuongeza kuwa, magaidi wasiopungua watatu wameuawa katika operesheni ya anga iliyofanywa na jeshi la Misri katika Rasi ya Sinai kwenye mpaka wa nchi hiyo na ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. 

Rasi ya Sinai ya kaskazini mwa Misri ni maficho ya magenge ya kigaidi likiwemo la Ansar Baytul Muqaddas ambalo mwezi Novemba 2014 lilitangaza utiifu wake kwa kundi la kigaidi la Daesh na  baadaye kujibadilisha jina na kujiita Wilaya ya Sinai.

Magaidi wakijiandaa kufanya mauaji dhidi ya mateka katika Rasi ya Sinai, kaskazini mwa Misri

 

Sehemu kubwa ya mashambulizi ya watu wenye silaha katika miezi ya hivi karibuni yamefanywa na kundi hilo katika Rasi ya Sinai.

Kundi hilo limekuwa likifanya mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya raia na maafisa wa serikali ya Misri. Mwezi Machi mwaka huu, magaidi hao waliua wanajeshi wanne wa Misri baada ya gari lao kukanyaga bomu la kutegwa ardhini katika Rasi ya Sinai. 

Duru za kijeshi ziliarifu kuwa, mripuko huo ulitokea yapata kilomita 20, kusini mwa mji wa al-Arish, kaskazini mwa Rasi ya Sinai. Habari zaidi zilisema kuwa, watu kadhaa walijeruhiwa katika shambulizi hilo la bomu.