Tahadhari ya UNCHR kuhusu kuibuka upya mapigano CAR
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i31174-tahadhari_ya_unchr_kuhusu_kuibuka_upya_mapigano_car
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia wakimbizi UNHCR limebainisha hofu yake kuhusu kuzuka upya mapigano katika baadhi ya sehemu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Jun 30, 2017 22:55 UTC
  • Tahadhari ya UNCHR kuhusu kuibuka upya mapigano CAR

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia wakimbizi UNHCR limebainisha hofu yake kuhusu kuzuka upya mapigano katika baadhi ya sehemu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Machafuko hayo mapya baina ya makundi ya ulinzi ya wananchi na makundi mengine ya wahalifu wabeba silaha yanaendelea katika miji ya Zemio, Bria na Kaga Bandaro Kusini na Kaskazini mwa CAR huku raia na wafanyakazi wa misaada wakilengwa. Andrej Mahecic msemaji wa UNHCR amesema baadhi ya nyumba karibu na ofisi ya UNHCR zimechomwa moto na watu zaidi ya 1000 wamekimbia wakazi yao. Amesema baadhi ya watu wamekimbilia hifadhi katika maeneo ya ibada huku wengine wakipata hifadhi katika ofisi za UNHCR.

Vita CAR vimewafanya watu zaidi ya 500,000 kuwa wakimbizi wa ndani na zaidi ya laki nne kutafuta hifadhi katika nchi jirani za Cameroon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Chad na Congo Brazaville.

Magaidi wa kundi la Anti Balaka huko Jamhuri ya Afrika ya Kati

Machafuko nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati yaliibuka mwaka 2013, baada ya waasi wa Seleka kumuondoka madarakani aliyekuwa rais wa taifa hilo, François Bozizé, huku mgogoro ukishadidi zaidi baada ya waasi wa Kikristo wenye kufurutu ada wa Anti-Balaka kuanzisha mauaji ya kutisha dhidi ya jamii ya Waislamu, ambapo maelfu ya watu waliuawa na wengine wengi kuwa wakimbizi. Hivi sasa kuna askari 10,000 wa kulinda amani katika nchi hiyo iliyo kati kati mwa bara la Afrika lakini hawajaweza kutuliza hali ya mambo na mapigano ya hapa na pale yangali yanaendelea.