HRW: yalaani jinai za kivita za makundi yenye silaha CAR
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i31390-hrw_yalaani_jinai_za_kivita_za_makundi_yenye_silaha_car
Jumuiya ya kutetea haki za binadamu ya Human Rights Watch (HRW) imetangaza kuwa, makundi ya wabeba silaha yamefanya jinai za kivita katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 05, 2017 23:37 UTC
  • HRW: yalaani jinai za kivita za makundi yenye silaha CAR

Jumuiya ya kutetea haki za binadamu ya Human Rights Watch (HRW) imetangaza kuwa, makundi ya wabeba silaha yamefanya jinai za kivita katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Ripoti iliyotolewa na Human Rights Watch imesema kuwa, makundi ya wanamgambo katika Jamhuri ua Afrika ya Kati yalifanya jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu katika kipindi cha kati ya mwaka 2014 na 2017. 

Ripoti hiyo imetolewa miezi kadhaa kabla ya kuanza mahakama maalimu ya kuchunguza jinai hizo katika mji mkuu wa nchi hiyo, Bangui. 

Human Rights Watch ambayo imesajili jinai zilizofanywa na wanamgambo wa zamani wa kundi la Seleka na wale wa kundi la Kikristo la Anti Balaka imesema katika ripoti hiyo kwamba, makundi hayo mawili yamekuwa yakitumia mbinu za kuua raia, kubaka wanawake na kuharibu vijiji.

Maelfu ya watu wamelazimika kukimbia makazi yao kutokana na ghasia CAR

Ripoti hiyo imesajili mauaji ya watu 566 na kusema hiyo ni sehemu ndogo ya jinai zilizofanywa na makundi ya wanamgambo wanaobeba silaha katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. 

Nchi hiyo ilitumbukia katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe baada ya kuondolewa madarakani serikali ya François Bozizé mwaka 2013.