Jul 23, 2017 13:49 UTC
  • 60 wauawa, kujeruhiwa katika mapigano ya makundi hasimu ya kigaidi Somalia

Kwa akali watu 20 wameuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa baada ya makundi hasimu ya wanamgambo kutandikana yenyewe kwa yenyewe katikati mwa Somalia.

Duru za kiusalama zinaarifu kuwa, mbali na watu 20 kuuawa, wengine zaidi ya 40 wamejeruhiwa baada ya wapiganaji wa vikosi vya Galmudug kupambana na genge la Ahlu Sunna wal-Jamaa, kati ya Ijumaa na jana Jumamosi.

Inaarifiwa kuwa, makundi hayo yanapigania udhibiti wa mji wa Herale, ulioko eneo la Galgadud, katikati ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Habari zaidi zinasema kuwa, licha ya wingu la taharuki kutanda, hali ya utulivu imeanza kushuhudiwa kwa kiasi fulani mjini hapo kuanzia jana, baada ya Rais Mohamed Abdullahi Farmajo wa Somalia kuzitaka pande hasimu kusitisha mapigano. Mji huo uko umbali wa kilomita 600 kaskazini mwa mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Moja ya magenge ya kigaidi nchini Somalia

Mazungumzo ya kuyapatanisha makundi hayo hasimu ya wabeba silaha yaligonga mwamba mwezi Aprili mwaka huu mjini Mogadishu.

Somalia ambayo inahesabiwa kuwa moja ya nchi masikini zaidi duniani imekuwa ikikabiliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe tokea mwaka 1991 kipindi ambacho aliyekuwa mtawala dikteta wa nchi hiyo, Siad Barre aling'olewa madarakani.

Tags