Tunisia: Hatukuwahi kukata mahusiano yetu na taifa la Syria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i32508-tunisia_hatukuwahi_kukata_mahusiano_yetu_na_taifa_la_syria
Waziri wa Mambo ya Nje wa Tunisia amesema kuwa, hakuna wakati ambapo mahusiano ya nchi yake na Syria yalikatika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 31, 2017 03:15 UTC
  • Tunisia: Hatukuwahi kukata mahusiano yetu na taifa la Syria

Waziri wa Mambo ya Nje wa Tunisia amesema kuwa, hakuna wakati ambapo mahusiano ya nchi yake na Syria yalikatika.

Khemaies Jhinaoui, amesisitiza kuwa Tunisia haikuafiki hatua ya kukata mahusiano na Damascus hapo mwaka 2012 na mahusiano ya kidiplomasia baina ya nchi mbili yameendelea kuwepo hadi sasa.

Jhinaoui amefafanua kuwa, hata kama Moncef Marzouki, rais wa zamani wa Tunisia alitangaza kukata mahuasiano na Syria, lakini uamuzi huo haukutekelezwa rasmi. Waziri wa Mambo ya Nje wa Tunisia amekiri kuwa, mahusiano ya kidiplomasia baina ya Syria na Tunisia hayajafikia katika ngazi ya mabalozi, lakini balozi ndogo za Damascus na Tunis zinaendelea na shughuli zao za kawaida.

Khemaies Jhinaoui, Waziri wa Mambo ya Nje wa Tunisia

Matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Tunisia yametolewa katika hali ambayo baadhi ya vyama vya siasa vya nchi hiyo na asasi za kitaifa za mrengo wa kushoto, vimekuwa vikiishinikiza serikali ya sasa kuanzisha mahusiano kamili ya kidiplomasia na Damascus.

Itakumbukwa kuwa Februari mwaka 2012, serikali ya wakati huo ya Tunisia kwa kushirikiana na nchi za Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi, ilitangaza kukata mahusiano kamili na serikali ya Syria.