HRW: 27 wauawa katika makabiliano ya polisi na waandamanaji DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i32990-hrw_27_wauawa_katika_makabiliano_ya_polisi_na_waandamanaji_drc
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema kwa akali watu 27 waliuawa katika makabiliano baina ya maafisa wa polisi na waandamanaji huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Jumatatu iliyopita.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 11, 2017 07:11 UTC
  • HRW: 27 wauawa katika makabiliano ya polisi na waandamanaji DRC

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema kwa akali watu 27 waliuawa katika makabiliano baina ya maafisa wa polisi na waandamanaji huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Jumatatu iliyopita.

Kwa mijibu wa shirika hilo, mauaji hayo yaliyotokea katika mji mkuu Kinshasa, na miji ya Matadi na Muanda ya kusini mwa nchi. 

Ida Sawyer , Mkurugenzi wa eneo la Afrika ya Kati wa Human Rights Watch amesema shiriki hilo linatoa mwito wa kufanyika uchunguzi huru ili kubaini wahusika wa mauaji hayo na kufikishwa mbele ya sheria watakaopatikana na hatia.

Awali iliarifiwa kuwa, watu 14 waliuawa kwa kupigwa risasi katika vurugu hizo zilizotokea Jumatatu iliyopita katika jiji la Kinshasa na mji wa Matadi, kusini mwa nchi hiyo. Kadhalika afisa mmoja wa polisi aliripotiwa kupoteza maisha katika ghasia hizo.

Ghasia za Jumatatu mjini Kinshasa

Kwa mujibu wa vyombo vya usalama vya DRC, ghasia hizo zilitokea kufuatia shambulio la wanachama wa kundi hilo la Kikristo katika jela kuu ya Kinshasa na maandamano yaliyofanywa na wanachama wengine wa kundi hilo dhidi ya Rais Joseph Kabila huko katika mji wa Matadi na katika mji wa Boma huko kusini magharibi mwa Kongo.

Jumatano iliyopita, polisi ya DRC iliwaonyesha hadharani na mbele ya vyombo vya habari watu 30 wa kundi la Bundu dia Kongo wanaotuhumiwa kupanga na kushiriki katika mashambulizi hayo ya Jumatatu katika mji mkuu wa nchi hiyo, kwa shabaha ya kuipindua serikali. 

Msemaji wa Polisi ya Kongo DR Kanali Ezéchiel Mwanamputu alisema watu hao ni magaidi waliofanya mauaji katika mji mkuu wa nchi siku ya Jumatatu.