UN: Mateso yaliyoratibiwa yanafanyika katika jela za Misri
Kamati ya Kimataifa ya Kupambana na Mateso ya Umoja wa Mataifa imeripoti habari kuhusu mateso yaliyoratibiwa yanayofanyika nchini Misri.
Ripoti ya kamati hiyo kuhusu mateso yaliyofanywa huko Misri tangu mwaka 2012 hadi sasa imesema kuwa, vitendo mbalimbali vya utesaji vinafanyika nchini Misri kwa mpango maalumu na kwa kusimamiwa na maafisa wa serikali ya nchi hiyo.
Kamati ya Kimataifa ya Kupambana na Mateso ya Umoja wa Mataifa pia imewataja baadhi ya wanajeshi wa Misri kuwa wanahusika na jinai hizo za mateso dhidi ya raia wa na imewataka viongozi wa Cairo kusitisha haraka mateso hayo yanayofanyika katika jela za nchi hiyo na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria wale wote wanaohusika.
Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch pia juzi lilitoa ripoti iliyosisitiza kuwa, mateso wanayopewa wafungwa wa kisiasa nchini Misri yanapasa kukomeshwa.
Human Rights Watch imeashiria masuala kama kupigwa, kushtuliwa kwa umeme, kubakwa na kutishwa kubakwa kuwa miongoni mwa mateso wanayofanyiwa wafungwa wa kisiasa katika jela za Misri.