Askari polisi 18 wa Misri wauawa Sinai; IS yatangaza kuhusika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i34225-askari_polisi_18_wa_misri_wauawa_sinai_is_yatangaza_kuhusika
Askari polisi wasiopungua 18 wa Misri wameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa wakati bomu liliporipuka karibu na msafara wa kikosi cha usalama katika Rasi ya Sinai kaskazini mwa nchi hiyo leo.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Sep 11, 2017 11:16 UTC
  • Askari polisi 18 wa Misri wauawa Sinai; IS yatangaza kuhusika

Askari polisi wasiopungua 18 wa Misri wameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa wakati bomu liliporipuka karibu na msafara wa kikosi cha usalama katika Rasi ya Sinai kaskazini mwa nchi hiyo leo.

Duru za usalama na hospitali zimethibitisha habari hiyo huku kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (IS) likitangaza kuhusika na shambulio hilo. Taarifa zinasema awali washambuliaji hao waliripua bomu kulenga msafara wa askari hao kisha wakawazingira na kuanza kuwafyatulia risasi.

Shambulio hilo lililotokea karibu na mji wa Arish, makao makuu ya jimbo la kaskazini la Sinai limesababisha askari wengine wanne pia kujeruhiwa akiwemo brigedia jenerali mmoja aliyekatika mguu pamoja na kuteketeza magari matatu ya deraya.

Eneo la Sinai limekuwa likishuhudia machafuko ambayo yanazidi kupamba moto kila uchao tangu jeshi la Misri lilipomwondoa madarakani Muhammad Morsi Julai mwaka 2013, rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini humo na mwanachama wa harakati kongwe ya Kiislamu ya Ikhawanul Muslimin. 

Mamia ya wanajeshi na askari polisi wameuawa hadi sasa katika hujuma na mashambulio yaliyotokea katika eneo hilo.

Wanamgambo wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (IS) katika Rasi ya Sinai

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri haijatoa taarifa kuhusiana na shambulio hilo la leo lakini shirika rasmi la habari la Misri MENA limemnukuu afisa wa ngazi za juu wa wizara hiyo akithibitisha kujiri kwake na maafa liliyosababisha.

Shirika hilo la habari limeripoti kuwa vikosi vya usalama lilifyatuliana risasi na wanamgambo karibu na eneo la tukio na kuwaua kadhaa miongoni mwao.

Kwa mujibu wa MENA, wafanyakazi wanne wa gari la kubebea wagonjwa pia wamejeruhiwa wakati wa ufyatulianaji risasi na kwamba vikosi vya usalama vinaendelea kuwaandama na kuwashambulia wanamgambo hao.../