Kiongozi wa zamani wa Ikhwanul Muslimin afariki dunia
Kiongozi mkuu wa zamani wa Harakati ya Ikhwanul Muslimin Mohammad Mahdi Akef, ameaga dunia Ijumaa mjini Cairo akiwa na umri wa miaka 89.
Akef ambaye alikuwa anashikiliwa gerezani aliaga dunia wakati akipata matibabu katika hospitali ya al-Qasr al-Aini baada ya afya yake kuzorota, amesema wakili wa Ikhwanul Muslimin Abdel-Maqsoud katika taarif kwa waandishi habari.
Binti yake marhum Alef, Alia, ametangaza kupitia ukurasa wake wa Facebook kuwa, "Baba yangu sasa yuko mikononi mwa Allah. Inna Lillah wa Inna Ilayhi Rajioun."
Akef alikuwa kiongozi mkuu wa Ikhwanul Muslimin baada ya kifo cha aliyemtangulia, Mamound al-Hudaibi mwaka 2004. Akef alijiuzulu wadhifa huo mwaka 2010 na nafasi yake ikachukuliwa na Mohammad Badie, ambaye hadi sasa anashikilia nafasi hiyo. Akef alitiwa mbaroni mwaka 2013 baada ya mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Mohammad Morsi, rais wa kwanza wa Misri kuchaguliwa kidemokrasia na ambaye pia ni mwanachama wa ngazi za juu wa Ikhwanul Muslimin.
Alikuwa amehukumuiwa kifungo cha miaka 25 gerezani lakini hukumu hiyo ilibatilishwa na wakati wa kifo chake kesi yake ilikuwa inaendelea.
Wimbi la kuishambulia Ikhwanul Muslimin na wafuasi wake lilianza mwaka 2013 baada ya wanajeshi wa Misri wakiongozwa na Jenerali Abdul Fattah al Sisi kuiondoa madarakani serikali iliyokuwa imechaguliwa na wananchi ya Mursi. Siasa za ukandamizaji na mbinyo wa kisiasa ulioandamana na ukatili dhidi ya wanaharakati wa kisiasa wa Misri, vinaonesha taswira mbaya na ya giza ya utawala wa Jenerali mstaafu Abdul Fattah al Sisi ambao baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema umekuwa mbaya zaidi kuliko hata ule wa kipindi cha dikteta wa zamani wa Misri, Hosni Mubarak.