Wahajiri 140 waokolewa baada ya boti zao kuzama Tunisia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i35087-wahajiri_140_waokolewa_baada_ya_boti_zao_kuzama_tunisia
Jeshi la Majini la Tunisia limefanikiwa kuokoa wahajiri wapatao 140, baada ya boti zao kuzama kusini mashariki mwa nchi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 01, 2017 11:45 UTC
  • Wahajiri 140 waokolewa baada ya boti zao kuzama Tunisia

Jeshi la Majini la Tunisia limefanikiwa kuokoa wahajiri wapatao 140, baada ya boti zao kuzama kusini mashariki mwa nchi.

Katika tukio la kwanza, raia 98 wa Tunisia wameokolewa baada ya boti yao kuanza kuzama katika pwani ya Kerkenah, kusini mashariki mwa nchi.

Kadhalika wahajiri haramu 43 wanazuiliwa na Jeshi la Majini la Libya, baada ya kuokolewa kutoka ndani ya boti nne za plastiki, katika eneo la pwani la Zarzis, kusini mashariki mwa nchi. 

Wahajiri walionusurika vifo

Vyombo vya usalama Tunisia vimewakamata wahajiri haramu 550 ndani ya mwezi uliopita wa Septemba, kulinganisha na 170 mwezi Agosti mwaka huu.

Aghalabu ya wahajiri hao haramu ambao kutokana na sababu za kiuchumi huamua kuzihama nchi zao kwa tamaa ya kwenda kutafuta kazi na maisha mazuri barani Ulaya, hutokea katika nchi za Nigeria, Eritrea, Niger, Somalia, Sudan, Gambia, Senegal, Mali, Morocco na Tunisia. 

Kwa mujibu wa Shirika la Uhamiaji Duniani, zaidi ya wahajiri elfu tano walipoteza maisha katika ajali za boti kwenye bahari ya Mediterranean, wakiwa katika safari hizo za kuogofya za kuelekea Ulaya.