Wanajeshi sita wa Misri wauawa katika shambulio la kigaidi Sinai
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i35607-wanajeshi_sita_wa_misri_wauawa_katika_shambulio_la_kigaidi_sinai
Watu wanaoaminika kuwa magaidi wakufurishaji wamewapiga risasi na kuwaua wanajeshi sita wa Misri katika eneo lililokumbwa na misukosuko la Rasi ya Sinai, kaskazini mwa nchi hiyo.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Oct 13, 2017 11:20 UTC
  • Wanajeshi sita wa Misri wauawa katika shambulio la kigaidi Sinai

Watu wanaoaminika kuwa magaidi wakufurishaji wamewapiga risasi na kuwaua wanajeshi sita wa Misri katika eneo lililokumbwa na misukosuko la Rasi ya Sinai, kaskazini mwa nchi hiyo.

Jeshi la Misri limetoa taarifa leo Ijumaa na kusema kuwa, 'magaidi waliokuwa na silaha wameshambulia kituo cha jeshi katika mji wa Arish kwa kutumia bunduki na mabomu ya mkononi na kuua wanajeshi sita."

Taarifa zinasema kuwa, wanajeshi wengine wanne wamejeruhiwa huku magaidi wawili wakiuawa katika ufyatulianaji risasi uliodumu kwa muda wa nusu saa.

Eneo hilo la kaskazini mwa Misri limekuwa uwanja wa mashambulizi ya makundi yenye silaha kwa miaka kadhaa sasa. Kundi hatari zaidi ni lile linalojiita Ansar Bait al-Muqaddas ambalo limetangaza utiifu wake kwa genge la kigaidi na la ukufurishaji la Daesh (ISIS).

Wanajeshi wa Misri wakiwa wakilinda doria

Eneo hilo halijawahi kuwa na utulivu tangu magenge ya kigaidi yaanzishe harakati zao mwaka 2013, baada ya jeshi la Misri kumuondoa madarakani kwa nguvu Mohamed Morsi, rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini Misri.

Mamia ya wanajeshi na askari polisi wameshauawa hadi hivi sasa katika hujuma na mashambulio yaliyotokea kwenye eneo hilo.