Wabunge Uganda wapewa 'hongo' ya mamilioni ya pesa kurefusha uongozi wa Museveni
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i35913-wabunge_uganda_wapewa_'hongo'_ya_mamilioni_ya_pesa_kurefusha_uongozi_wa_museveni
Msemaji wa Bunge la Uganda amesema kila Mbunge wa nchi hiyo amepewa shilingi milioni 29 za nchi hiyo, sawa na dola elfu 8 za Marekani, kufanikisha muswada wa kuondoa kikomo cha umri wa kugombea urais.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 24, 2017 10:11 UTC
  • Wabunge Uganda wapewa 'hongo' ya mamilioni ya pesa kurefusha uongozi wa Museveni

Msemaji wa Bunge la Uganda amesema kila Mbunge wa nchi hiyo amepewa shilingi milioni 29 za nchi hiyo, sawa na dola elfu 8 za Marekani, kufanikisha muswada wa kuondoa kikomo cha umri wa kugombea urais.

Chris Obore amesema pesa hizo tayari zimewekwa kwenye akaunti za benki za Wabunge hao wiki hii, ambazo watatumia katika shughuli za kupokea maoni ya wakazi wa maeneobunge yao kuhusu muswada huo.

Amesema kwa jumla serikali imetumia shilingi bilioni 13 dola milioni 3.3, kuwapa wabunge 445 wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki, kitendo ambacho kimewaghadhabisha sana wakosoaji wa serikali na wananchi walalahoi.

John Baptist Nambeshe, mmoja wa wabunge wanaopinga muswada huo ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa: "Hii ni rushwa ya wazi na haingii akilini kudai kuwa ni fedha za kushughulikia masuala ya Bunge."

 

Rais Yoweri Museveni wa Uganda

Watu wawili wameuawa, huku makumi ya wengine wakitiwa mbaroni kwa kushiriki maandamano ya kupinga muswada huo.

Muswada wa kuondoa kipengee cha umri wa kugombea urais kiliwasilishwa katika bunge la Uganda mwezi uliopita na hivi sasa wabunge wanajadiliana na wananchi wa kawaida kutaka kujua maoni yao. 

Rais Yoweri Museveni mwenye umri wa miaka 73, ambaye amekuwa madarakani kwa zaidi ya miongo mitatu, kisheria hafai kuwania tena urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2021 kwa sababu katiba ya Uganda imeainisha miaka 75 kuwa kikomo cha umri wa mtu anayetaka kugombea urais.