Oct 27, 2017 04:10 UTC
  • Polisi ya Ethiopia yaua watu 5 katika eneo la Oromiya

Watu wasiopungua 5 wameuawa baada ya polisi ya Ethiopia kuwafyatulia risasi waandamanaji katika mji mmoja wa eneo lenye ghasia na machafuko ya mara kwa mara la Oromiya.

Polisi waliwafyatulia risasi waandamanaji waliofunga barabara ya mji wa Limbo ulioko umbali wa kilomita 130 magharibi mwa Addis Ababa. Raia hao walikuwa wakiandamana kulalamikia uhaba wa sukari.

Watu walioshuhudia wanasema polisi waliwavyatulia risasi waandamanaji hao na kwamba watu watano wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Msemaji wa serikali ya eneo hilo , Addisu Arega Kitessa amethibitisha kwamba watu kadhaa wameuawa katika machafuko hayo lakini amekataa kutoa maelezo zaidi. 

Maandamano ya kabila la Oromo, Ethiopia

Eneo la Oromiya lilikumbwa na machafuko makubwa katika kipindi cha kati ya mwaka 2015 na 2016. Karibu watu mia saba waliuawa katika machafuko hayo ya kulalamikia  mipango ya serikali ya kutwaa ardhi ya kabila la Oromo. Wapinzani wa serikali ya Addis Ababa na watetezi wa haki za binadamu wanaituhumu serikali ya Ethiopia kwamba inakanyaga haki za binadamu, kubinya uhuru wa kisiasa na kuyabagua makundi na baadhi ya makabila.  

Tags