Nov 01, 2017 08:02 UTC
  • Waandamanaji karibu 30 watiwa mbaroni mashariki mwa Kongo DR

Duru za polisi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimearifu kuwa watu karibu 30 wametiwa nguvuni katika maandamano dhidi ya serikali katika mji wa Goma makao makuu ya mkoa wa Kivu ya Kaskazini huko mashariki mwa nchi hiyo.

Duru hizo zimearifu kuwa watu 28 wamekamatwa katika maandamano ya mji wa Goma wakipinga kuendelea kuwepo madarakani Rais Joseph Kabila. Polisi ya Kongo imesisitiza kuwa waandamanaji hao wanatuhumiwa kumiliki silaha kinyume cha sheria na kwamba tayari wamefikishwa mbele ya mwendesha mashtaka wa kijeshi.  

Habari zinasema kuwa raia wanne na polisi mmoja wameuawa katika maandamano na mapigano yaliyojiri kati ya waandamanaji na askari usalama huko Goma. Watu wengine tisa walitiwa mbaroni katika maandamano yaliyofanywa  jana katika mkoa wa Kivu ya Kaskazini dhidi ya Rais Kabila.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilikumbwa na mgogoro wa kisiasa kufuatia kuakhirishwa mara mbili uchaguzi wa Rais na kuendelea kung'ang'ania madarakani Rais Joseph Kabila. 

Maandamano Goma dhidi ya Rais Joseph Kabila 

Uchaguzi mkuu umepangwa kufanyika nchini humo kabla ya kumalizika mwaka huu chini ya makubaliano yaliyofikiwa kati ya serikali ya Kinshasa na mrengo wa upinzani. Hata hivyo imeelezwa kuwa huenda zoezi hilo lisifanye kama ilivyopangwa hasa kwa kuzingatia kuwa Tume ya Uchaguzi ya Kongo mwezi Julai mwaka huu ilitangaza kuwa kuna uwezekano uchaguzi huo usifanyike mwaka huu kutokana na matatizo ya bajeti na machafuko yanayoendelea nchini humo.

Tags