Nov 11, 2017 07:23 UTC
  • Magaidi wawili watiwa mbaroni kaskazini mwa Morocco

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Morocco imetangaza habari ya kutiwa mbaroni magaidi wawili kaskazini mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Xinhua, vikosi vya ulinzi vya Morocco vimewatia mbaroni wanachama hao wawili wa genge la kigaidi na la ukufirshaji la Daesh (ISIS) katika mji wa Fas wa kaskazini mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Morocco, magaidi hao wawili walikuwa na nia ya kutega mabomu katika maeneo ya watalii na yenye watu wengi mjini Fas.

Morocco iko karibu mno na bara Ulaya ni njia inayotumiwa sana kuingia na kutoka kiurahisi katika mabara mawili ya Afrika na Ulaya

 

Tarehe 25 Oktoba mwaka huu pia, vikosi vya usalama vya Morocco viliwatia mbaroni magaidi wanne wanachama wa genge la ISIS waliokuwa mbioni kufanya shambulio la kigaidi.

Baada ya kusambaratishwa katika nchi za Iraq na Syria, magaidi wa Daesh wamekuwa wakirejea katika nchi zao hasa za kaskazini mwa Afrika na za barani Ulaya, suala ambalo limezusha wasiwasi mkubwa kwa nchi hizo. 

Magaidi hao wamekuwa wakifanya mashambulizi pia katika nchi za Ulaya ambazo zilikuwa mstari wa mbele kuwalea na kuwapa mafunzo ya kijeshi kwa lengo la kuvuruga usalama wa nchi za Kiislamu za Mashariki ya Kati hasa za Iraq na Syria, ingawa hata hivyo inaonekana kuwa baada ya kushindwa njama hizo, magaidi hao wamekuwa tishio kubwa kwa nchi hizo hizo za Ulaya ambazo zilikuwa zinawaunga mkono.

Tags