Chad yakanusha madai ya Marekani kuwa rais wake alipokea rushwa
Serikali ya Chad imekadhibisha vikali tuhuma zilizotolewa na Marekani kwamba Rais Idriss Deby wa nchi hiyo ya Kiafrika alipokea rushwa ya dola milioni 2 za Marekani ili kutoa haki ya kustafidi na mapato ya mafuta ya nchi hiyo.
Taarifa ya serikali ya N'Djamena imesema tangu nchi hiyo ianze kuzalisha mafuta kiongozi wa taifa hilo amekuwa na uwazi wa hali ya juu na kufanya jitihada za kuhakikisha kuwa maliasili hiyo inapata usimamizi mzuri.
Taarifa hiyo imesema Chad ni nchi huru yenye mamlaka ya kujitawala na kwamba inakosoa vikali kitendo cha Marekani na baadhi ya mashirika yanayofanya juu chini kuchafua jina la taifa hilo na ofisi ya rais wake.
Marekani iliwakamata aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Chad na katibu wa zamani wa masuala ya ndani wa Hong Kong kwa tuhuma za kumpa Rais Deby mlungula wa dola milioni 2 ili kuidhinisha kupewa kandarasi ya mafuta kampuni moja ya China.
Hii sio mara ya kwanza kwa Marekani na Chad kujikuta katika msuguano wa kidiplomasia.
Mapema mwezi uliopita wa Oktoba, Rais Deby alitoa amri ya kufungwa ubalozi wa Marekani nchini humo likiwa ni jibu kwa amri ya uhajiri iliyotolewa na Rais Donald Trump wa Marekani ya kupiga marufuku kuingia nchini humo raia wa nchi kadhaa ikiwemo Chad.