Nov 24, 2017 14:15 UTC
  • Watu 235 wauawa katika shambulizi dhidi ya msikiti huko Sinai, Misri

Kwa akali watu 185 wameuawa na makumi ya wengine wamejeruhiwa katika shambulizi la kigaidi dhidi ya msikiti mmoja katika Peninsula ya Sinai nchini Misri.

Duru za polisi nchini humo zimesema genge la kigaidi limeushambulia Msikiti wa al-Rawdhah ulioko katika mji wa Bir al-Abd, yapata kilomita 40 kutoka mji wa Arish, makao makuu ya mkoa wa Sinai Kaskazini.

Habari zinasema kuwa, magaidi hao waliokuwa wamejizatiti kwa silaha wameshambulia kwa bomu msikiti huo, na kisha kuanza kuwafytulia risasi ovyo waumini wa Kiislamu waliokuwa wanashiriki hotuba na Sala ya Ijumaa katika msikiti huo.

Baadhi ya mashuhuda wamenukuliwa na shirika la habari la Reuters wakisema kuwa, magaidi hao wamemeonekana wakizifyatulia risasi pia ambulensi zilizokuja kuwabeba majeruhi wa hujuma hiyo.

 

Masjidu-Rraudhah, eneo la Sinai, Misri

Msemaji wa Wizara ya Afya ya Misri amesema watu wasiopungua 80 wamejeruhiwa katika shambulio hilo kinyama.

Rais Abdulfattah al-Sisi wa Misri sanjari na kulaani hujuma hiyo, ameitisha mkutano wa dharura na vyombo vya usalama huku akitangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa, kufuatia ukatili huo wa magaidi.

Hadi tunaenda mitamboni, hakuna kundi lolote lililotangaza kuhusika na shambulizi hilo linalotajwa kubwa zaidi katika kipindi cha zaidi ya miaka mitatu, tangu vyombo vya usalama vya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika vianze kukabiliana na magenge ya kigaidi na kitakfiri.

Hujuma ya kigaidi dhidi ya kanisa nchini Misri miezi michache iliyopita

Eneo hilo la kaskazini mwa Misri limekuwa uwanja wa mashambulizi ya makundi yenye silaha yenye mafungamano na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh tangu mwaka 2013, baada ya jeshi la Misri kumuondoa madarakani kwa nguvu Mohamed Morsi, rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini Misri.

Tags