Dakta Shein aapishwa kushika hatamu ya uongozi Zanzibar
(last modified Thu, 24 Mar 2016 16:23:47 GMT )
Mar 24, 2016 16:23 UTC
  • Rais wa Zanzibar
    Rais wa Zanzibar

Rais mteule wa Zanzibar, Dakta Ali Mohamed Shein ameapishwa leo kushika hatamu ya uongozi visiwani humo. Dakta Shein ameapishwa leo kufuatia ushindi alioupata Jumapili iliyopita wa kura 299,982 sawa na asilimia 91.4 ya kura zote halali 328,327 zilizopigwa katika uchaguzi marudio.

Akihutubia taifa baada ya kula kiapo, Dakta Shein amesema serikali yake italinda haki za raia, kuhimiza uwajibikaji na usawa pasipo kubagua mtu yeyote. Katika sherehe hizo zilizofanyika kwenye uwanja wa Amaan mjini Unguja, Rais Shein pia ameahidi kuunda serikali itakayounganisha Wazanzibar na kwamba atahakikisha misingi ya Muungano iliyowekwa wakati wa kuasisiwa kwake inadumishwa. Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC ilimtangaza mgombea wa kiti cha rais kupitia Chama cha Mapinduzi CCM, Dakta Ali Muhammed Shein kuwa mshindi wa uchaguzi wa marudio uliofanyika Jumapili visiwani humo. Vyama 9 kati ya 14 vilivyoshiriki katika uchaguzi uliofutwa, kikiwemo Chama cha Wananchi CUF vimesusia uchaguzi huo wa marudio. Mbali na CCM, vyama vingine vilivyoshiriki uchaguzi wa jana ni pamoja na TLP, ACT Wazalendo, SAU na ADA-TADEA. Kinachosubiriwa kwa sasa ni kuona hatua itakayochukuliwa na viongozi wa chama cha CUF, ambao wamekuwa wakishikilia kuwa mgombea wao Maalim Seif Sharif Hamad ndiye aliyekuwa mshindi halali katika uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana 2015.

Tags