Iran na Mauritania kuimarisha uhusiano wa pande mbili
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i37413-iran_na_mauritania_kuimarisha_uhusiano_wa_pande_mbili
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Mauritania zimeeleza juu ya hamu na utayarifu wao wa kuimarisha uhusiano wa pande mbili katika nyuga mbalimbali.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 10, 2017 03:31 UTC
  • Iran na Mauritania kuimarisha uhusiano wa pande mbili

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Mauritania zimeeleza juu ya hamu na utayarifu wao wa kuimarisha uhusiano wa pande mbili katika nyuga mbalimbali.

Hayo yalibainika katika kikao kilichofanyika jana Jumamosi, kati ya Mohammad Omrani, Balozi wa Iran nchini Mauritania na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo ya kaskazini magharibi mwa Afrika, Isselkou Ould Ahmed Izid Bih mjini Nouakchott.

Wawili hao wamesisitizia udharura wa kuimarishwa uhusiano wa pande mbili hususan katika nyuga za siasa, uchumi, biashara, utamaduni na sayansi.

Balozi wa Iran nchini Mauritania amebainisha kuwa, nchi hizo mbili za Kiislamu zina fursa ya kuboresha ushirikiano wao wa kibunge.

Bendera ya Mauritania

Mwanadiplomasia huyo wa Iran kadhalika amekabidhi barua ya mwaliko kutoka kwa Ali Larijani, Spika wa Bunge la Iran kwa mwenzake wa Mauritania, kushiriki mkutano wa 13 wa Muungano wa Mabunge ya Kiislamu.

Duru ya 12 ya kikao cha Muungano wa Mabunge ya Kiislamu kilichofanyika mjini Bamako, mji mkuu wa Mali Januari mwaka huu ilitoa wito wa kufanyika juhudi za duru za kieneo na kimataifa kwa ajili ya kuhakikisha Wapalestina wanapatiwa haki zao za kisheria hususan haki ya kurejea makwao wakimbizi wa Kipalestina, kukombolewa maeneo yote ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu na kuundwa nchi huru ya Palestina mji mkuu wake ukiwa Baytul Muqaddas.