Dec 15, 2017 04:15 UTC
  • Vita dhidi ya Boko Haram vyazidi kuungwa mkono nchni Nigeria

Wakuu wa mikoa tofauti ya Nigeria jana walikubaliana na mpango wa kutenga kitita cha dola bilioni moja kwa ajili ya kuisaidia Serikali Kuu kupambana na genge la kigaidi la Boko Haram.

Mapambano dhidi ya kundi la wakufurishaji la Boko Haram yameongezeka sana katika wiki za hivi karibuni baada ya genge hilo la kigaidi kuongeza kasi ya kutumia wanawake na watoto wadogo kufanya mashambulizi ya mabomu katika miji ya kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Maiduguri, eneo lililoshuhudia mashambulizi mengi zaidi ya Boko Haram nchini Nigeria

 

Shirika la habari la Associated Press limeripoti kuwa, wakuu 36 wa mikoa ya Nigeria wamekubaliana na mpango wa kuingizwa dola bilioni moja katika mfuko maalumu wa kuisaidia Serikali Kuu kupambana na Boko Haram.

Fedha hizo zitatumika kununulia vifaa vya kiusalama na masuala ya kilojistiki pamoja na kukusanya taarifa za siri na za kijasusi kuhusiana na genge hilo.

Hata hivyo hadi hivi sasa kumekuwa kukifanyika ufisadi mkubwa katika manunuzi ya silaha za kupambana na Boko Haram kiasi kwamba mshauri wa usalama wa taifa wa zamani wa nchi hiyo anakabiliwa na tuhuma za wizi wa mamia ya mamilioni ya dola zilizotengwa kwa ajili ya kununua silaha za kupambana na Boko Haram nchini Nigeria.

Genge hilo la wakufurishaji lilizuka nchini Nigeria mwaka 2009 na hadi hivi sasa limeshasababisha zaidi ya watu 20 elfu kuuawa na wengine milioni 2 na laki sita kuwa wakimbizi huko kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Tags