Afrika Kusini kuteremsha hadhi ya ubalozi wake huko Israel
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i37905-afrika_kusini_kuteremsha_hadhi_ya_ubalozi_wake_huko_israel
Afrika Kusini imesema kuwa itateremsha hadhi ya mahusiano yake ya kidiplomasia huko Israel ikiwa ni radiamali kwa uamuzi wa Marekani wa kuutambua mji wa Quds kuwa ni mji mkuu wa Israel.
(last modified 2026-04-24T06:29:55+00:00 )
Dec 21, 2017 12:48 UTC
  • Afrika Kusini kuteremsha hadhi ya ubalozi wake huko Israel

Afrika Kusini imesema kuwa itateremsha hadhi ya mahusiano yake ya kidiplomasia huko Israel ikiwa ni radiamali kwa uamuzi wa Marekani wa kuutambua mji wa Quds kuwa ni mji mkuu wa Israel.

Chama tawala cha Kongresi ya Taifa cha Afrika Kusini (ANC) kilitangaza uamuzi huo jana jioni katika mkutano wake huko Johannesburg. Mkutano wa taifa wa chama tawala ANC, ambao unatambulika kama kikao cha  ngazi ya juu cha kutoa maamuzi ya chama kwa sauti moja umeamua kuchukuliwa haraka na bila ya masharti yoyote hatua ya kushusha hadhi ya ubalozi wa Afrika Kusini huko Israel na kuwa ofisi tu ya mahusiano.

Taarifa ya ANC imesema kuwa uamuzi huo umechukuliwa kwa lengo ya kutuma ujumbe wa kivitendo kwa wananchi wanaokandamizwa wa Palestina na pia kutuma ujumbe wa wazi kwa Israel kwamba unapaswa kugharimika kwa ukiukaji wake wa haki za binadamu na kukiuka sheria za kimataifa. Uamuzi wa Afrika Kusini wa kushusha hadhi ya ubalozi wake huko Tel Aviv awali ulipendekezwa katika mkutano wa sera wa chama hicho mwezi Julai mwaka huu. 

Mapema mwezi huu Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kuwa Washington imeutambua rasmi mji wa Quds kama mji mkuu wa utawala wa Kizayuni na kwamba ameagiza serikali yake kuanza mchakato wa kuuhamisha ubalozi wa nchi ihyo kutoka Tel Aviv hadi katika mji huo mtakatifu; hatua iliyokabiliwa na radiamali kali na kupingwa vikali na  nchi na taasisi mbalimbali za kimataifa. 

Maandamano ya kuiunga mkono Quds Tukufu, kibla cha kwanza cha Waislamu