Watu wasiopungua 6 wauawa katika mlipuko kaskazini mashariki mwa Nigeria
Watu wasiopungua sita wameuawa na wengine 13 kujeruhiwa katika shambulio la kujitoa muhanga lililotekelezwa sokoni katika kijiji kimoja karibu na mji wa Maiduguri jimboni Borno kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Mamluki wa kundi la kigaidi la Boko Haram ndiye alitekeleza shambulio hilo la kujitoa muhanga kwa kujilipua hapo jana huko Maiduguri. Mji wa Maiduguri ni kitovu cha mapigano na makabiliano kati ya vikosi vya serikali na magaidi wa kundi la kitakfiri la Boko Haram.
Mwaka 2009 kundi hilo lilianza kubeba silaha na kutekeleza hujuma na mashambulizi mbalimbali huko kaskazini mwa Nigeria na kisha kueneza mashambulizi hayo katika nchi za Niger, Chad na kaskazini mwa Cameroon. Kundi la kigaidi la Boko Haram limeuwa watu zaidi ya elfu 20 huko Nigeria, Cameoon, Niger na Chad na kuwafanya raia wengine zaidi ya milioni mbili kuwa wakimbizi tangu mwaka 2009 hadi sasa.
Kushindwa serikali za eneo khususan serikali ya Nigeria kukabiliana na kundi la kigaidi la Boko Haram kumepelekea kuzorota vita dhidi ya kundi hilo la kitakfiri.