Jan 01, 2018 04:21 UTC
  • Al-Shabaab yadai kuua askari 5 wa Amisom, Somalia

Kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab linadai kwamba limeua askari watano wa Kikosi cha Askari wa Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika Amisom katika mlipuko wa bomu uliotokea mjini Mogadishu jana Jumapili.

Hata hivyo vyombo vya habari nchini humo vinasema shambulio hilo lililolenga msafara wa magari ya Amisom limeua mtu mmoja na kujeruhi wengine watatu.

Mashuhuda wanasema hujuma hiyo ya kigaidi imelenga wanajeshi wa Burundi, ambao wamekuwa wakiendeshea operesheni zao katika eneo la Jaalle Siyaad.

Polisi ya Somalia imesema mpita njia aliyeuawa ni raia na kwamba hakuna askari yeyote aliyeuawa au kujeruhiwa kwenye shambulio hilo. 

Wanajeshi wa Amisom nchini Somalia

Kikosi cha Amisom ambacho kiliundwa kupitia azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na ambacho kimekuwa kikiisaidia serikali ya Somalia kupambana na magaidi wa kundi la al Shabab tangu mwaka 2007, hakijatoa radimali yoyote kufuatia shambulio hilo.

Hivi karibuni kikosi hicho kilianza kupunguza idadi ya askari wake nchini humo na kusisitiza kwamba kufikia tarehe 31 Disemba (Jana Jumapili) askari 1000 wa kikosi hicho wangekuwa wameondoka katika ardhi ya Somalia.

Tags