Kuendelea machafuko ya kikabila nchini Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i38487-kuendelea_machafuko_ya_kikabila_nchini_nigeria
Katika mashambulizi mapya ya kikabila nchini Nigeria, watu wa kabila la Fulani wameshambulia eneo la Tif na kuua zaidi ya watu 50 wa eneo hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 03, 2018 23:03 UTC

Katika mashambulizi mapya ya kikabila nchini Nigeria, watu wa kabila la Fulani wameshambulia eneo la Tif na kuua zaidi ya watu 50 wa eneo hilo.

Samuel Ortom, meya wa jimbo la Benue sambamba na kuthibitisha shambulizi hilo na kuikosoa serikali ya Nigeria kwa kutowalinda wakulima wa eneo la Tif, amesema, kabla ya kujiri shambulizi hilo aliwakumbusha viongozi wa ngazi ya juu serikalini juu ya uwepo wa vitisho vya wafugaji wa kabila la Fulani dhidi ya wakazi wa eneo hilo. Hili ni shambulizi la mara kadhaa kufanywa na wafugaji wa kikabila katika miezi ya hivi karibuni nchini humo.

Miili ya watu waliouawa katika mashambulizi ya kikabila

Hata kama machafuko ya kikabila nchini Nigeria ni yenye historia ya muda mrefu, lakini ukame, upungufu wa chakula, ongezeko la tofauti za kidini na kimadhehebu, ubaguzi wa serikali na kushindwa serikali kuu kudhibiti hali ya mambo, ni mambo yanayochangia kuongezeka vita vya kikabila ndani ya taifa hilo la magharibi mwa Afrika. Hivi sasa utumiwaji wa ardhi na vyanzo vya maji ni changamoto kubwa inayoyakabili maeneo mengi ya nchi hiyo. Ukame wa hivi karibuni na kupungua maeneo ya malisho ya mifugo, kumewafanya watu wa kabila la Fulani kukabiliwa na hali ngumu kila siku. Suala hilo limepelekea pia kuongezeka malalamiko na mapigano ya kikabila katika maeneo mengi ya Nigeria.

Mauaji ya kikabila Nigeria

Licha ya kwamba, Nigeria ina utajiri wa mafuta na gesi huku ikiwa inaingiza pato la fedha za kigeni kutokana na vyanzo hivyo, lakini mwenendo wa kushuka bei ya mafuta katika soko la dunia, kumeibua wimbi la ufisadi na harakati za magenge yanayojishughulisha na magendo katika kujaribu kujikimu na hali ya uchumi, huku wakazi wa maeneo mengi ya nchi hiyo wakiendelea kudidimia katika dimbwi la umasikini na ukosefu wa ajira. Machafuko na ongezeko la kila uchao la harakati za kigaidi za genge la ukufurishaji la Boko Haram katika maeneo ya kaskazini mwa nchi, ni sababu nyingine ambayo kwa upande mmoja imepelekea kupungua uwekezaji ndani ya taifa hilo, na kwa upande mwingine kuongezeka bajeti ya kudhamini mahitaji ya kijeshi katika kupambana na wanachama wa kundi hilo la kigaidi. Kuhusiana na suala hilo, Goodwin Obbaski, mmoja wa magavana wa majimbo ya Nigeria ametangaza kwamba, jumla ya magavana 36 wamefanikiwa kutenga kiasi cha dola bilioni moja kutoka akaunti maalumu za pato la uzalishaji mafuta, kwa ajili ya kununua zana za kivita, kilojestiki na ukusanyaji wa taarifa za kiintelejensia.

Kukosekana maeneo ya malisho ya mifugo, chanzo cha migogoro

Baadhi ya weledi wa mambo wanaamini kwamba, siasa za ubaguzi ambazo zimekuwa zikitekelezwa na serikali ya Abuja katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni dhidi ya baadhi ya makabila na madhehebu nchini na kadhalika kushindwa kwake kudhibiti hali ya mambo ni sababu kuu ya kuendelea mapigano na mashambulizi ya kikabila nchini humo. Hali hiyo imewafanya watu wa kabila la Fulani waamini kwamba serikali imewatenga. Hata kama nchini Nigeria kuna zaidi ya makabila 250, lakini hila za makundi ya kigaidi yanayoendesha harakati zao nchini zimefanikiwa kuwavutia vijana wengi wa kabila la Fulani na kuwafanya wawashambulie watu wa makabila mengine kwa madai ya kutetea haki zao zinazokanyagwa na serikali. Siku chache zilizopita Rais Muhammadu Buhari wa nchi hiyo bila kuashiria udhaifu wa serikali yake katika kudhamini usalama wa makabila, alisema kuwa haifai kuruhusiwa kutekelezwa vitendo viovu ambavyo vinaweza kulitumbukiza taifa hilo katika mgogoro mkubwa.