Libya yawatia mbaroni wahajiri 81 kutoka Somalia, Ethiopia na Eritrea
Vyombo vya usalama mashariki mwa Libya vimewakamata makumi ya wahajiri raia wa Somalia, Eritrea na Ethiopia, ambao walikwepa mtego wa magendo ya binadamu.
Ahmed al-Arifi, afisa wa ngazi za juu katika Idara ya Kupambana na Uhamiajia Haramu nchini humo amesema wahajiri hao wamekamatwa katika eneo la Zueitina mjini Benghazi na karibuni hivi watarejeshwa katika nchi zao.
Amesema wahajiri zaidi ya 5,600 walikamatwa na kurejeshwa makwao mashariki mwa Libya mwaka jana 2017, ikilinganishwa na takriban elfu tatu mwaka juzi.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, Libya iliwarejesha nchini kwao wahajiri haramu wapatao 142 raia wa Guinea, ikiwa ni katika jitihada za kupunguza msongamano wa wahamiaji haramu wanaozuiliwa katika vituo mbali mbali nchini humo.
Ripoti za Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR zinaonyesha kuwa, kuna wahajiri elfu 18 katika vituo na jela zilizoko chini ya usimamizi wa serikali ya Libya.
Hivi karibuni televisheni ya CNN ilirusha hewani kanda ya video inayoonesha namna wahajiri wa Kiafrika wanavyopigwa mnada sokoni na kuuzwa kama watumwa huko Libya, aghalabu yao wakiuzwa kwa dola zisizozidi 400 za Marekani.