Kuundwa kundi jipya la ISIS barani Afrika
Baada ya kuangamizwa genge la wakufurishaji la Daesh (ISIS) katika nchi za Iraq na Syria, sasa magenge yenye misimamo mikali ya kigaidi yametangaza kuunda muungano mpya unaojulikana kwa jina la "Kundi la Daesh katika Jangwa la Sahara."
Kundi hilo jipya ambalo limeundwa na vikundi kadhaa vyenye misimamo mikali litakuweko katika eneo la pembe tatu la mpaka wa Mali, Burkina Faso na Niger kwa ajili ya kukabiliana na jeshi la nchi tano za eneo la Sahel linalojulikana kwa jina la G5. Kundi hilo jipya la Daesh linaongozwa na mtu anayejiita kwa jina la Adnan Abu al Walid al Sahrawi ambaye ni muhusika mkuu wa mashambulizi ya kigaidi katika eneo la Sahel barani Afrika.
Kuna sababu kadhaa zinazolifanya eneo la Sahel Afrika kukabiliwa na hatari ya kujipenyeza makundi ya kila namna ya kigaidi. Kuangamizwa genge la kigaidi la Daesh huko Syria na Iran kumelilazimisha kundi hilo kutafuta maeneo mengine ya kupeleka wanamgambo wake. Hali ya machafuko na kukosekana serikali yenye nguvu nchini Libya na machafuko katika nchi kama ya Mali, ni miongoni mwa mambo ambayo yamelifanya kundi hilo kuyaona maeneo hayo kuwa maficho salama kwa wanamgambo wake. Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria, Abdul Qadir Msaheel amesema: Raia wa kigeni wanachama wa Daesh (ISIS) wanatumwa kwa wingi nchini Libya na kaskazini mwa Afrika hivi sasa jambo ambalo linaonesha namna genge hilo la kigaidi lilivyo na nia ya kupanua shughuli zake katika maeneo hayo.
Sababu nyingine inayoyafanya magenge ya kigaidi yapate nguvu za kujipenyeza katika maeneo hayo ni ukosefu wa kazi, ukame, njaa, umaskini na ukata wa kupindukia. Mambo hayo yanawafanya wakazi wa maeneo hayo kuwa wepesi sana kurubuniwa na magenge ya kigaidi na kukabidhi maeneo yao kwa makundi ya kigaidi. Magenge ya kigaidi yanatumia vibaya ukosefu wa utulivu na pia umaskini wa kiuchumi na kiutamaduni katika baadhi ya nchi ili kujipenyeza na kufanya vitendo vya kigaidi. Wachambuzi wa mambo wanasema, hiyo ndiyo sababu inayopelekea kuwa vigumu sana kuyamaliza magenge ya kigaidi kama Boko Haram, Daesh na al Shabab lililotangaza utiifu wake kwa mtandao wa wakufurishaji wa al Qaida barani Afrika.

Baadhi ya weledi wa mambo wanasema kuwa, kuna nchi kadhaa za Magharibi zinayaunga mkono magenge ya kigaidi katika eneo hilo kwani kadiri hatari ya ugaidi inavyoongezeka barani Afrika ndivyo nchi hizo za Magharibi zinavyozidi kupata kisingizio cha kujizatiti kijeshi katika bara hilo. Ushahidi unaotolewa na wachambuzi hao ni jinsi mauaji na mapigano yanavyoendelea katika nchi kama za Mali na Jamhuri ya Afrika ya Kati licha ya kuweko wanajeshi wa mkoloni Ufaransa katika nchi hizo kama ambavyo weledi hao wanaashiria pia namna Ufaransa ilivyojitokeza haraka kudai kukiunga mkono kikosi cha G5 barani Afrika. Ushahidi mwingine ni ule uliotolewa na afisa wa zamani wa kijasusi wa Marekani, Edward Snowden ambaye alifichua kuwa, mashirika ya kijasusi ya Marekani, Uingereza na utawala wa Kizayuni yalikuwa na mchango mkubwa katika kuundika genge la kigaidi la Daesh (ISIS).
Kiujumla ni kuwa, kuna mambo mengi yanalifanya eneo la Sahel Afrika kuwa windo rahisi la magenge ya kigaidi na ya wakufurishaji. Ismail Sharafi, kamishna wa usalama na amani wa Umoja wa Afrika ametahadharisha kuhusu hatari ya kurejea barani Afrika wanachama elfu sita wenye misimamo mikali wa genge la Daesh na kusema: Nchi za Afrika zinapaswa kujipanga vizuri kukabiliana na hatari hiyo.
Ukweli wa mambo ni kwamba hatari ya kupata nguvu magenge ya kigaidi barani Afrika ni janga kwa dunia nzima. Wachambuzi wa mambo wanazishauri nchi za Afrika kuongeza ushirikiano wao wa kijeshi na kijasusi, kuweka pembeni ugomvi wa ndani na kuelekeza nguvu zao zote katika kukabiliana na hatari ya magaidi hao ambao jinai walizofanya Iraq na Syria zinathibitisha kuwa hawa chembe ya ubinadamu.