Takwa la Wamisri la kuondolewa madarakani Rais wa Misri el-Sisi
-
Rais wa Misri
Kwa mara nyingine tena raia wa Misri wamefanya maandamano ya kutaka kuondolewa madarakani Rais Abdel Fattah el-Sisi wa nchi hiyo. Wamisri katika mji wa Minya na kufanya maandamano, walimtaka rais huyo kuondoka madarakani mara moja.
Waandamanaji hao ambao ni wafuasi wa rais Muhammad MOrsi aliyeondolewa madarakani na makamanda wa jeshi, na kufunga barabara za mji huo wametaka pia kuachiliwa huru MOrsi kutoka jela pamoja na wafungwa wengine wa kisiasa wanaoendelea kuzuiliwa katika korokoro za kijeshi za nchi hiyo. Aidha waandamanaji hao walitoa nara kama vile, "Al-Sisi lazima aondoke madarakani" "Morsi ni Rais halali" na "Utawala wa kisheria uliopinduliwa lazima urejee madarakani." Katika sehemu nyingine waandamanaji wametaka pia kuboresha hali ya maisha ya raia wa nchi hiyo na kupunguzwa mfumuko wa bei ndani ya taifa hilo. Waandamanaji wamesisitiza kuwa, serikali ya Cairo imeshindwa kufikia malengo ya mapinduzi ya tarehe 25 Januari na pia kuimarisha misingi ya uhuru na demokrasia kwa ajili ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. Takwa la wananchi wa Misri limetolewa katika hali ambayo wiki iliyopita, mahakama ya nchi hiyo ilimuhukumu Muhammad Morsi na viongozi wengine 12 wa Harakati ya Ikhwanul Muslimin, kifungo cha miaka 20 jela, katika kesi iliyohusu ikulu ya rais. Kwa mujibu wa mahakama hiyo, tuhuma dhidi ya Morsi na viongozi hao 12 wa Ikhwanul Muslimin, zinahusu ukatili dhidi ya waandamanaji katika faili la ikulu ya Misri. Wakati huo huo, kabla ya kutolewa hukumu hiyo, harakati hiyo ya Ikhwanul Muslimin ililaani hukumu zinazotolewa dhidi ya wanachama wake na kumtuhumu Rais Abdel Fattah el-Sisi kufanya ukandamizaji kupitia vyombo vya mahakama vya nchi hiyo. Ukandamizaji mkubwa dhidi ya wapinzani wa serikali ya rais huyo umesababisha asasi za kimataifa za haki za binaadamu ukiwemo Umoja wa Mataifa kuufananisha utawala huo na ule uliopita wa dikteta Hosni Mubarak. Alkhamisi iliyopita Zeid Ra'ad Al Hussein, Kamishna Mkuu wa Haki za Binaadamu wa Umoja wa Mataifa alitoa ripoti inayoelezea kuendelea ukandamizaji na kamatakamata dhidi ya watetezi wa haki za binaadamu nchini Misri, na kukosoa sheria inayohalalisha suala hilo na kufungwa asasi za kiraia, sheria ambayo imekuwa ikifanya kazi tangu mwaka 2011 nchini humo. Pamoja na hayo, upinzani wa wananchi bado ungali unaendelea siku hadi siku huko Misri. Kukosekana mazingira mazuri ya kiuchumi na kisiasa, kumeongeza sana mashinikizo kwa wananchi. Mgogoro wa uchumi nchini Misri umepelekea magazeti kadhaa kufunga ofisi zao huku mengine yakilazimika kuendeleza shughuli zake kupitia Intaneti tu. Mashinikizo ya kiuchumi dhidi ya raia wa nchi hiyo na pia malalamiko yao dhidi ya serikali, kulimfanya Rais Abdel Fattah el-Sisi Jumatano iliyopita aamue kuteua mawaziri 10 wapya pamoja na kufanya mabadiliko ya mawaziri wa fedha na uwekezaji nchini humo.