Masalafi wapigwa marufuku kutoa mihadhara misikitini Misri
-
Sheikh Jabir Taayi'i
Wizara ya Waqfu ya Misri imetangaza kuwa imewapiga marufuku masalafi na wakufurishaji kupanda kwenye mimbari za misikiti kadhaa ya nchi hiyo na kutoa mihadhara ya kidini.
Sheikh Jabir Taayi'i, Mkuu wa kitengo cha masuala ya dini cha Wizara ya Waqfu ya Misri ameliambia gazeti la Misr-alyaum kuwa wizara hiyo imewapiga marufuku masalafi kutoa mihadhara ya kidini katika misikiti minne mikubwa ya nchi ambayo imekuwa vituo vya kuwashawishi watu kujiunga na masalafi. Ameongeza kuwa hatua hiyo imechukuliwa baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi.
Sheikh Jabir Taayi'i amesisitiza kuwa Wizara ya Waqfu inachukua hatua kali za kukabiliana na makundi yenye misimamo ya kufurutu ada na masalafi.
Mkuu huyo wa kitengo cha masuala ya dini cha Wizara ya Waqfu ya Misri ameashiria umuhimu linaopewa suala la kupambana na masalafi katika wizara hiyo na kubainisha kuwa wafanya tablighi msikitini hivi sasa ni wafanyakazi na waajiriwa wa serikali.
Takwimu zinaonyesha kuwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh linaloyakalia maeneo kadhaa ya ardhi za Syria na Iraq limevutia vijana wengi kutoka nchi za kaskazini mwa Afrika zikiwemo Tunisia, Libya na Misri. Vijana hao hushawishika kutokana na mitazamo ya kufurutu mpaka ya Kisalafi na ya Kiwahabi.../