Jan 23, 2018 07:37 UTC
  • Ripoti ya UN yataka askari wa kulinda amani watumie nguvu

Ripoti ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa imetoa pendekezo kwa askari wa kulinda amani wa umoja huo kutumia 'nguvu' kuzima tishio dhidi yao wanapolazimika kufanya hivyo wakiwa katika operesheni zao.

Hii ni kufuatia ongezeko la mauaji ya askari wa kofia buluu wa Umoja wa Mataifa katika sehemu mbali mbali duniani wanakolinda amani.

Ripoti hiyo imekabidhiwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres na timu ya wataalamu iliyoongozwa na Luteni Jenerali Carlos Alberto Cruz, kamanda wa zamani wa UN katika nchi za Haiti na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Mamia ya askari wa kimataifa wa kudumisha amani wa UN wameshauawa katika hujuma za magenge ya kigaidi na ya wabeba silaha katika nchi mbali mbali kama vile Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mali, Somalia na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Mwaka jana pekee, askari 56 wa UN waliuawa wakiwa katika operesheni zao za kulinda amani katika nchi bali mbali duniani.

Askari wa Tanzania nchini Kongo

Itakumbukwa kuwa, askari 15 wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)  na watano wa Kongo DR waliuawa mwanzoni mwa mwezi uliopita wa Disemba, katika kambi ya Semuliki mkoani Kivu Kaskazini kufuatia hujuma ya waasi wa ADF wa Uganda. 

Wanajeshi wa Tanzania na Kongo walikuwa sehemu ya askari 3,000 wa timu ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa nchini Kongo MONUSCO yenye askari kutoka Tanzania, Malawi na Afrika Kusini.

Tags