Feb 03, 2018 03:37 UTC
  • Wapinzani wa serikali wazidi kutiwa mbaroni nchini Sudan

Idadi ya wakuu wa vyama vya siasa, wanaharakati wa kisiasa na waandishi wa habari waliotiwa mbaroni nchini Sudan tangu yalipoanza malalamiko ya wananchi ya kulalamika kupanda bei ya bidhaa imeongezeka nchini humo.

Shirika la habari la IRNA limetangaza kuwa, maafisa usalama wa Sudan wamewaweka kizuizini viongozi kadhaa wa vyama vya upinzani kama njia ya kukabiliana na malalamiko ya wananchi wanaopinga marekebisho ya kiuchumi ya serikali ya nchi hiyo.

Saleh Mahmoud al Mahami, mjumbe wa kamati kuu ya chama cha Kikomunisti na Fadhlullah Barmat Nasser, Naibu Mwenyekiti wa chama cha Umma ni miongoni mwa viongozi wa kisiasa waliotiwa mbaroni na maafisa usalama wa Sudan siku ya Alkhamisi.

Maandamano ya wananchi nchini Sudan

 

Wanasiasa wengine waliotiwa mbaroni na serikali ya Sudan tangu katikati ya Januari 2018 ni pamoja na Mohamed Mukhtar al-Khatib, Katibu Mkuu wa chama cha Kikomunisti, Omar Al-Daghir, mkuu wa chama cha Congress, Sara Nafdallah, Katibu Mkuu wa chama cha Umma na  Abraham Al-Amin pamoja na Mohamed Abdullah al-Dawma viongozi wengine wa chama cha Umma kama njia ya kukabiliana na malalamiko hayo ya wananchi.

Wapinzani wa serikali ya Sudan wamesema kuwa, kutiwa mbaroni wakuu wa vyama vya upinzani ni hatua zisizo na maana kwani kadiri serikali inavyowaweka kizuizini viongozi hao ndivyo upinzani dhidi ya serikali unavyozidi kuwa mkubwa.

Malalamiko ya wananchi yalianza katikati ya mwezi Januari 2018 baada ya serikali ya Sudan kuanza kufanya marekebisho magumu ya kiuchumi kama njia ya kutekeleza masharti ya Mfuko wa Kimataifa wa Fedha (IMF).

Tags