Maandamano dhidi ya Israel nchini Tunisia
Wananchi wa Tunisia wameandamana kuunga mkono rasimu ya sheria ya kupiga marufuku uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Waandamanaji waliokuwa na hasira wamejumuika katika mji mkuu Tunis kulalamikia hatua ya wabunge wanaofungamana na chama tawala kupinga sheria ya kupiga marufuku hatua yoyote ya kuwa na uhusiano wa kawaida na Israel.
Katika maandamano hayo ambayo pia yaliwajumuisha baadhi ya wabunge, wanaharakati wa kisiasa na haki za binadamu, washiriki walitaka kuendelezwe mashinikizo dhidi ya serikali na wabunge wa chama tawala ili sheria hiyo ya kupiga marufuku uhusiano na Israel ipitishwe.
Sheria hiyo ilipendelezwa na Chama cha Mrengo wa Wananchi Tunisia na imeungwa mkono na wananchi waliowengi katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Rafqi Ghanmi mmoja kati ya viongozi wa harakati hiyo ameashiria kuenea ushawishi na mtandao wa kijasusi wa utawala wa Kizyauni wa Israel nchini Tunisia na kusema: "Hivi sasa Tunisia iko katika kipindi cha kihistoria na wananchi kwa kushadidisha malalamiko yao hawataruhusu sheria hiyo ya kupiga marufuku uhusiano na Israel ipuuzwe na bunge."