Ethiopia yanunua hisa za Bandari ya Berbera Somaliland
(last modified Fri, 02 Mar 2018 07:51:46 GMT )
Mar 02, 2018 07:51 UTC
  • Ethiopia yanunua hisa za Bandari ya Berbera Somaliland

Serikali ya Ethiopia imenunua asilimia 19 ya hisa za Bandari ya Berbera iliyoko katika Jamhuri iliyojitangazia uhuru ya Somaliland nchini Somalia.

Shirika la Dubai la DP World linalosimamia na kuendesha bandari hiyo limetangaza kuwa litabakia na asilimia 51 ya hisa huku nchi mwenyeji Somalilanda ikisalia na asilimia 30.

Shirika hilo la Umoja wa Falme za Kiarabu lilichukua asilimia 65 ya hisa ya bandari hiyo ilipozinduliwa mwaka 2016, ikiwa ni sehemu ya mradi wa pamoja na serikali ya Somaliland; makubaliano yanayotazamiwa kuendelea kuwepo kwa kipindi cha miaka 30.

Muamala huu wa kibiashara kati ya Imarati, Ethiopia na Somaliland unafanyika wiki moja baada ya Djibouti kufuta makubaliano yake na shirika la DP World la UAE, la kuendesha shirika la kusafirisha mashehena ya Doraleh, jambo ambalo limeitia hamaki Imarati.

Ramani inayozionyesha nchi za Pembe ya Afrika

Sio vibaya kukumbusha hapa kuwa, mwaka uliopita, mpango wa Imarati wa kutaka kujenga kambi yake ya kijeshi huko Somaliland ulipingwa vikali na nchi jirani zikiwemo Ethiopia na Djibouti.

Jamhuri ya Somaliland ilijitenga na Somalia mwaka 1991 na kisha kuitangaza Hargeisa kuwa mji  mkuu wake.