Ethiopia yaituhumu Eritrea kuwa inataka kuvuruga usalama wake
(last modified Mon, 19 Mar 2018 03:16:23 GMT )
Mar 19, 2018 03:16 UTC
  • Ethiopia yaituhumu Eritrea kuwa inataka kuvuruga usalama wake

Ethiopia imemtuhumu jirani yake Eritrea kuwa inataka kuvuruga usalama wake kwa kuyaunga mkono yale iliyoyaita makundi "haribifu" katika kipindi hiki ambapo sheria ya hali ya hatari inatekelezwa nchini humo.

Kwa mujibu wa televisheni ya taifa ya Ethiopia, baraza la kipindi cha hali ya hatari linaloongoza nchi hiyo limefanikiwa kunasa silaha za makundi "haribifu" yaliyokuwa yakijaribu kuingiza kimagendo silaha hizo nchini humo kupitia mpakani.

Hizo ni shutuma za kwanza kutolewa dhidi ya Eritrea tangu Ethiopia ilipotangaza sheria ya hali ya hatari tarehe 18 ya mwezi uliopita wa Februari kufuatia kujiuzulu waziri mkuu wa nchi hiyo Hailemariam Desalegn.

Hali hiyo ya hatari inayotazamiwa kuendelea hadi mwezi Agosti mwaka huu ni ya pili kutangazwa nchini Ethiopia katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Taswira za matukio tofauti wakati wa vita vya mpakani kati ya Ethiopia na Eritrea

Mnamo mwezi Agosti mwaka jana, serikali ya Addis Ababa iliondoa sheria ya hali ya hatari iliyokuwa imewekwa kwa muda wa miezi 10 baada ya mamia ya watu kuuawa katika maandamano dhidi ya serikali ya kudai uhuru mkubwa zaidi wa kisiasa.

Itakumbukwa kuwa Ethiopia na jirani yake Eritrea ziliingia vitani mara mbili kwa sababu ya mzozo wa mpaka katika kipindi cha kuanzia mwaka 1998 hadi 2000. Eritrea, ambayo awali ilikuwa sehemu ya Ethiopia ilijitenga na nchi hiyo na kujitangazia uhuru wake rasmi mwaka 1993.../