Watu 17 wafariki dunia katika tufani kali nchini Madagascar
Kwa akali watu 17 wameripotiwa kupoteza maisha katika tufani kali nchini Madagascar.
Idara ya kitaifa ya kukabiliana na majanga hatari na vifo nchini Madagascar imetoa ripoti ikisema kwamba tufani kali ya eneo la Ikweta iliyoikumba nchi hiyo imesababisha hasara kubwa ya mali na roho na kwamba hadi kufikia Jumapili ya jana, zaidi ya watu elfu 15 wamejeruhiwa. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, tufani hiyo kali ya Ikweta iliyoanza siku ya Ijumaa tarehe 16 Machi, ilikikumba kisiwa cha Masoala, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo na kisha kuendelea kuvuma kutoka mashariki mwa kisiwa hicho kuelekea upande wa kusini.
Aidha siku ya Jumamosi iliyopita, tufani hiyo iliendelea kuvuma hadi katika miji ya Mandritsara na Soanierana Ivongo. Inafaa kuashiria kwamba, Madagascar ni kati ya nchi masikini zaidi duniani, ambapo miaka 10 iliyopita ilikumbwa pia na kimbunga na tufani kali na kusababisha hasara kubwa. Mwezi Januari mwaka huu nchi hiyo pia ilikumbwa na kimbunga cha Ava na kusababisha kwa akali watu 51 kufariki dunia na wengine 22 kutoweka. Mbali na hayo mwezi Machi mwaka jana pia Madagascar ilikumbwa na kimbunga cha Enawo ambacho kilisababisha vifo vya watu 78 na wengine wengi kujeruhiwa.