Misri yamfunga kifungo cha nyumbani Hisham Ganinah
Duru za habari nchini Misri zimearifu kuwa, Mkuu wa Idara ya Mahesabu ya Taifa aliyeuzuliwa siku chache zilizopita na Rais Abdel Fattah el-Sisi, amewekwa katika kizuzi cha nyumbani nchini humo.
Habari za kuaminika zinasema kuwa, Hisham Ganinah, amewekwa kizuizini nyumbani kwake huku maafisa usalama wakiendelea kuizingira nyumba yake. Aidha maafisa usalama nchini humo wamemzuia Ganinah kukutana na kiongozi yeyote. Hisham Ganinah alifutwa kazi na Rais Abdel Fattah el-Sisi tarehe 28 mwezi uliopita wa Machi. Baadhi ya duru za habari nchini Misri zimeripoti kuwa, Ganinah amezuiliwa pia kufanya safari nje ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. Itakumbukwa kuwa, Ganinah ndiye kiongozi pekee kati ya viongozi waliochaguliwa na rais wa zamani wa nchi hiyo Muhammad Morsi, aliyeendelea kubakia madarakani hata baada ya kuja serikali mpya inayoongozwa na makamanda wa jeshi chini ya Abdel Fattah el-Sisi hapo mwaka 2013. Kwa muda mrefu sasa Ganinah na baadhi ya vyombo vya habari nchini Misri wamekuwa wakilengwa na vyombo vya usalama vya serikali.