Sisitizo la Rais wa Tunisia la kujitawala kikamilifu nchi hiyo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i42780-sisitizo_la_rais_wa_tunisia_la_kujitawala_kikamilifu_nchi_hiyo
Rais wa Tunisia ametangaza kuwa nchi hiyo inajitawala kikamilifu licha ya mashinikizo na matatizo yote yaliyopo na kueleza kuwa Tunisia inajivunia historia yake ya mapambano, kuwa huru na mafanikio iliyopata katika miongo kadhaa iliyopita licha ya matatizo na mashinikizo yote ya ndani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 07, 2018 22:22 UTC
  • Sisitizo la Rais wa Tunisia la kujitawala kikamilifu nchi hiyo

Rais wa Tunisia ametangaza kuwa nchi hiyo inajitawala kikamilifu licha ya mashinikizo na matatizo yote yaliyopo na kueleza kuwa Tunisia inajivunia historia yake ya mapambano, kuwa huru na mafanikio iliyopata katika miongo kadhaa iliyopita licha ya matatizo na mashinikizo yote ya ndani.

Ni miaka saba sasa mbapo Rais wa Tunisia anatangaza suala la kujitawala kamili nchi hiyo baada ya mapambano ya ukombozi ya wananchi; ambapo nchi hiyo pia sawa na nchi nyingine nyingi katika eneo kama Algeria kwa miaka kadhaa sasa imekuwa chini ya mashinikizo ya siasa za kikoloni za Ufaransa huku sekta mbalimbali za nchi hiyo zikidhibitiwa na Wafaransa. Kwa kadiri kwamba moja ya malengo ya harakati za ukombozi za wananchi wa Tunisia mwaka 2011 lilikuwa ni kujitoa chini ya uistikbari wa viongozi mabeberu ili kujitawala katika nyanja zote.

Mapinduzi ya wananchi wa Tunisia mwaka 2011

Hivi sasa baada ya kupita zaidi ya miaka saba tangu kuanza vuguvugu hilo la harakati za mapinduzi ya wananchi wa Tunisia licha ya kuwa baadhi ya malengo ya harakati hizo yamefikiwa, lakini baadhi ya wananchi wa nchi hiyo wana wasiwasi kuhusu kuendelea nchi yao kuwa tegemezi kwa Ufaransa. Kiasi kwamba Rais Beji Caid Essebsi wa Tunisia pia amekiri katika hotuba yake kuwa pamoja na mafanikio yote yaliyopatikana nchini humo, baadhi ya shakhsia na makundi ya nchi hiyo yangali yana shaka kuhusiana na suala la kujitegemea na kujitawala nchi hiyo kutoka kwa nchi koloni ya Ufaransa. 

Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema kuwa pamoja na mafanikio iliyoyapata Tunisia katika nyanja mbalimbali, Ufaransa ingali ni tishio kuu kwa suala la kujitegema na kujitawala nchi hiyo. Tishio hilo linaonekana kuwa kubwa zaidi katika kipindi cha sasa ambapo hali mbaya ya kiuchumi ya Tunisia na haja yake ya kushirikiana na pande nyingine katika sekta mbalimbali za kiuchumi inawapa fursa bora zaidi Wafaransa kuwa na ushawishi nchini humo. Ziara nyingi za viongozi wa Ufaransa na masisitizo yao kuhusu kuwa na ushirikiano wa pamoja na Tunisia, ni miongoni mwa dalili zinazotajwa katika uwanja huo.

Hii ni kwa sababu Paris inahesabiwa kuwa mshirika mkubwa zaidi wa kiuchumi wa Tunisia huku ikiendesha asilimia 70 ya biashara yote ya Tunisia. 

Tunisia inakabiliwa na matatizo chungu nzima katika sekta za kiuchumi na kijamii licha ya jitihada zote zinazofanywa. Katika sekta ya kiuchumi, nchi hiyo inakabiliwa na mfumuko wa bei na umaskini. Kuhusiana na suala hilo Marwan Abbasi Gavana wa Benki Kuu ya Tunisia anasema: Mfumuko wa bei unazidi kuongezeka nchini humo kwa kiasi kikubwa na tatizo hili litashindwa kudhibitiwa iwapo hatua za lazima za kuzuia mfumuko huo wa bei hazitachukuliwa. Matatizo hayo yamevuruga hali ya uthabiti na kuibua malalamiko ya wananchi nchini humo kiasi kwamba raia wengi wanataka kufanyike marekebisho khususan katika sekta ya kiuchumi. 

Dakta Marwan Abbasi, Gavana wa Benki Kuu ya Tunisia

Hii ni katika hali ambayo Tunisia inatazamia kuendesha uchaguzi wa mabaraza ya miji karibu mwezi mmoja ujao. Uchaguzi huo ni wa kwanza kuwahi kufanyika huko Tunisia baada ya mapinduzi ya mwaka 2011; na ni uchaguzi wenye umuhimu mkubwa. Kwa msingi huo viongozi wa Tunisia wanafanya kila wawezalo kuandaa mazingira mazuri ili uchaguzi huo ufanyike kwa amani na kutayarisha ramani ya njia iliyo wazi na huru ili wananchi waweze kushiriki kwa wingi katika uchaguzi huo. Sisitizo la Essebsi kuhusu kujitawala Tunisia pia linapasa kutathminiwa katika uwanja huo.