Wizara ya Ulinzi ya Misri: Tumeua magaidi 65 Sinai Kaskazini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i4285-wizara_ya_ulinzi_ya_misri_tumeua_magaidi_65_sinai_kaskazini
Wizara ya Ulinzi ya Misri imetangaza kuwa, vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo vimeua magaidi wasiopungua 65 katika mkoa wa Sinai Kaskazini.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 02, 2016 11:58 UTC
  • Wizara ya Ulinzi ya Misri: Tumeua magaidi 65 Sinai Kaskazini

Wizara ya Ulinzi ya Misri imetangaza kuwa, vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo vimeua magaidi wasiopungua 65 katika mkoa wa Sinai Kaskazini.

Wizara hiyo imetoa taarifa na kusema kuwa, vikosi vya ulinzi vya Misri kwa kushirikiana na jeshi la anga na polisi vimeshambulia maficho ya magaidi hao katika viunga vya miji ya Rafah na Sheikh Zuweid na kuua wanamgambo wasiopungua 65.

Hata hivyo taarifa hiyo haikusema operesheni hizo zimefanyika lini. Watu walioshuhudia katika mji wa al Arish wamesema kuwa, wameona ndege za kivita aina ya F-16 na helikopta aina ya Apachi za jeshi la Misri zkiruka katika anga ya mji humo siku ya Jumatano na kusikia milio ya risasi na miripuko.

Aidha Wizara ya Ulinzi ya Misri imetangaza kuwa, jeshi la anga la nchi hiyo limefanya operesheni katika maeneo ya magharibi mwa nchi hiyo na kuangamiza magari 12 ya wafanya magendo katika mpakani mwa Misri na Libya.

Tangu mwaka 2013 wakati jeshi lilipofanya mapinduzi yaliyomng'oa madarakani rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia, Muhammad Morsi, hadi hivi sasa, Misri imo kwenye machafuko yasiyoisha hususan katika rasi ya Sinai ya kaskazini mwa nchi hiyo. Mamia ya wapinzani wa serikali ya Misri wameshauawa na maelfu ya wengine kusukumwa jela kwa kuipinga serikali ya majenerali wa kijeshi ya nchi hiyo.