Wapinzani waandamana Madagascar kupinga sheria mpya za uchaguzi
Maelfu ya wapinzani nchini Madagascar wameandamana leo katika mji mkuu Antananarivo wakilalamikia sheria mpya za uchaguzi wa Rais zilizopasishwa na Bunge la nchi hiyo.
Waandamanaji hao waliokuwa wamebeba mabango na maberamu walisikika wakipiga nara kupinga sheria mpya za uchaguzi.
Wapinzani hao wanasema kuwa, sheria hizo mpya zimepasishwa ili kuumzuia mgombea wao Marc Ravalomanana ambaye amewahi kuwa Rais wa nchi hiyo kushiriki katika uchaguzi ujao.
Wapinzani hao leo walikusanyika katikati mwa mji mkuu Antananarivo wakipinga kile walichosema kuwa njama za kutaka kuumzuia Marc Ravalomanana asigombee urais katika uchaguzi ujao.
Polisi mjini Antananarivo imelazimika kutumia mabomu ya gesi ya kutoa machozi ili kuwatawanya waandamanaji hao ambao walisababisha pia shughuli katika mji huo kukwama kwa masaa kadhaa.
Watu kadhaa wanaripotiwa kujeruhiwa katika harakati za polisi kuwatawanya waandamanaji hao.
Mbunge mmoja wa upinzani ameinyooshea serikali kidole cha lawama na kukosoa vikali mashambulio ya vikosi vya usalama dhidi ya wafuasi wa upinzani.
Uchaguzi ujao wa Rais nchini Madagascar umepangwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.
Marc Ravalomanana alishika madaraka ya Madagascar mwaka 2002 na mwaka 2009 aliondolewa madarakani na aliyekuwa meya wa mji mkuu wa nchi hiyo, Andry Rajoelina, suala ambalo liliitumbukiza nchi hiyo katika machafuko ya ndani yaliyoendelea kwa miaka kadhaa.