Kambi ya upinzani Madagascar yamtaka rais wa nchi ajiuzulu
Kambi ya upinzani nchini Madagascar imemtaka Rais na Waziri Mkuu wa nchi hiyo wajiuzulu na kusisitiza kwamba haitashiriki tena katika mazungumzo juu ya mgogoro wa kutunga sheria mpya ya uchaguzi.
Makamu Mwenyekiti wa chama cha upinzani cha Tiako Ia Madagasikara (TIM) amesema kambi ya upinzani haitashiriki tena katika mjadala wa sheria mpya ya uchaguzi.
Hanitra Razafimanantsoa amesisitiza kuwa kwa sasa kambi ya upinzani inamtaka Rais Hery Rajaonarimampianina na waziri wake mkuu wajiuzulu.
Kambi ya upinzani inasema sheria mpya ya uchaguzi huenda ikatumiwa na serikali kumzuia kiongozi wa upinzani, Marc Ravalomanana kugombea kiti cha rais kwa madai ya kuhusika na makosa ya jinai katika kesi iliyosikilizwa dhidi yake akiwa uhamishoni baada ya jaribio la mapinduzi.
Ravalomanana aliyewahi kuwa rais wa Madagascar anashirikiana na aliyemrithi kiti hicho, Andy Rajoelina, kupinga marekebisho na sheria za uchaguzi yanayoungwa mkono na Rais wa sasa wa nchi hiyyo, Hery Rajaonarimampianina.
Jumatano iliyopita Jumuiya ya Maendeleo na Ustawi wa Kusini mwa Afrika SADC ilimtaka mjumbe wake maalumu katika mzozo wa Madagascar, Joaquin Chissano kuelekea katika nchi hiyo kwa ajili ya kutuliza mivutano ya sasa. Hata hivyyo baadhi ya wanasiasa wa kambi ya upinzani wamekataa kumtambua rasmi rais huyo wa zamani wa Msumbiji kama mpatanishi katika mzozo wa kisisa wa nchi hiyo.