Upinzani Uganda waijia juu serikali kwa mauaji ya viongozi wa Kiislamu
Viongozi wa upinzani nchini Uganda wameitaka serikali ya Kampala kutoa ripoti kuhusu mauaji na kamatakamata dhidi ya viongozi na wahubiri wa Kiislamu katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Hussein Kyanjo, Katibu Mkuu wa zamani wa chama cha upinzani cha Justice Forum (JEEMA) amesema viongozi wengi wa Waislamu nchini Uganda wanazuiliwa na vyombo vya dola kwa miaka mingi pasina na kufikishwa mahakamani au hata serikali kutoa taarifa kuhusu tuhuma zinazowakabili.
Kyanjo aliyasema hayo jana katika kikao na waandishi wa habari mjini Kampala na kuongeza kuwa, "Sheria zetu zinawapa watuhumiwa haki ya kuwa na wakili na pia kutembelewa na watu wa familia, lakini mshukiwa anapokuwa ni Muislamu, inakuwa vigumu sana kupata wakili au hata kuonana na watu wake."
Matamshi ya chama hicho cha upinzani Uganda yanakuja wiki moja baada ya maafisa wa polisi kuvamia msikiti mmoja karibu na Soko la Usafi, ambapo washukiwa wawili waliuawa kwa kupigwa risasi huku wengine 36 wakitiwa mbaroni. Kwa mujibu wa polisi, operesheni hiyo iliwaokoa watoto 94 na wanawake 18 waliokuwa wameshikwa mateka.
Mwaka jana pia polisi wa Uganda walivamia Msikiti wa Nakasero na kuwatia mbaroni Waislamu 11 waliokuwepo hapo, kwa tuhuma za uhalifu. Hii ni katika hali ambayo, mapema mwaka jana, polisi ya Uganda iliomba radhi kutokana na kitendo cha maafisa wake wa Kikosi cha Kupambana na Ugaidi (JATT) kufanya msako mkali katika Msikiti huo wa Nakasero ulioko jijini Kampala na kukamata watu kadhaa wakiwemo wasimamizi na walinzi wa msikiti huo mwishoni mwa mwaka 2016.
Kadhalika mwaka jana maafisa usalama walivamia msikiti mwingine katika katika eneo la Kiwatule na kuwatia nguvuni Waislamu 13 wakiwemo wahubiri wanane wa Kiislamu wenye asili ya Asia (Tabligh), ingawaje baadaye waliachiwa huru.