Kenya yaomboleza ajali ya ndege ndogo iliyoua watu 10
Rais Uhuru Kenyatta analiongoza taifa la Kenya katika kuomboleza vifo vya watu 10 waliopoteza maisha katika ajali ya ndege iliyotokea katika eneo la milima ya Aberdares mjini Kinangop kaunti ya Nyandarua, kaskazini mwa mji mkuu Nairobi.
Katika taarifa, Kenyatta amesema: Nimehuzunishwa sana na habari ya ajali ya ndege karibu na eneo la Kinangop. Simanzi na maombi yangu yako pamoja na familia za wahanga wa ajali hii. Nawaombea subira na faraja familia na marafiki wa wahanga wa ajali hiyo katika wakati huu mgumu wa majonzi.
Ndege ndogo aina ya Cessna C208 ya shirika la FlySax ambayo ilikuwa inatoka mjini Kitale kuelekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta JKIA jijini Nairobi ilitoweka kwenye rada saa 11:20 jioni siku ya Jumanne, baada ya kuruka kutoka uwanja mdogo wa ndege wa Kitale kaunti ya Trans-Nzoia saa 10:05.

Ndege hiyo iliyokuwa na abiria wanane na rubani mmoja na msaidizi wake ni moja ya ndege zinazosimamiwa na kampuni ya ndege ya East Africa Safari Air Express.
Paul Maringa, Katibu katika Wizara ya Uchukuzi nchini Kenya amesema ukungu mzito na baridi kali katika eneo hilo la miinuko ndiyo iliyosababisha shughuli ya kutafuta mabaki ya ndege hiyo kuwa ngumu.