Indhari kuhusu uingiliaji wa utawala haramu wa Kizayuni eneo la Darfur, Sudan
(last modified Mon, 18 Jun 2018 02:32:59 GMT )
Jun 18, 2018 02:32 UTC
  • Indhari kuhusu uingiliaji wa utawala haramu wa Kizayuni eneo la Darfur, Sudan

Chama cha Kongresi ya Kitaifa nchini Sudan kimetahadharisha kuhusiana na uingiliaji wa utawala haramu wa Israel eneo la Darfur huko Sudan kwa lengo la kuibua machafuko nchini humo.

Ali al-Haj, katibu mkuu wa chama hicho amesema kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel sambamba na kufanya uingiliaji huo kwa kushirikiana na pande kadhaa, kwa mara nyingine unakusudia kuwasha moto wa vita katika eneo la Darfur kwa ajili ya kufikia malengo yake mapya katika eneo hilo. Kwa muda sasa utawala wa Kizayuni kupitia siasa na malengo ya kupenda kujitanua, umekuwa ukilikodolea macho bara la Afrika ambapo umekuwa ukiendesha shughuli zake za kisiasa, kiuchumi, kijeshi na kiusalama katika nchi nyingi za bara hilo kwa kificho na hata kwa wazi.

Makundi ya wabeba silaha yanayofadhiliwa na Israel huko Darfur

Kufuatilia malengo ya kiuchumi, kujitanua katika uga wa kimataifa kwa lengo la kuvutia kura katika Umoja wa Mataifa na kufikia vyanzo na akiba ya kistratijia vya nchi za Kiafrika, ni miongoni mwa malengo yanayofuatiliwa na utawala wa Kizayuni kwa kujipenyeza ndani ya nchi za bara hilo. Katika uwanja huo, viongozi wa utawala haramu wa Israel, wamekuwa wakishiriki shughuli za kiuchumi na uwekezaji katika sekta tofauti za kiuchumi, kuuza silaha na zana nyingine za kijeshi, kutoa mafunzo ya kijeshi na kadhalika kuchochea tofauti  za ndani zikiwemo tofauti za kidini na kikabila katika nchi nyingi za Afrika. Hivi karibuni Shlomo Amar, kiongozi wa Kiyahudi alinukuliwa akisema: “Israel imehusika na miamala ya mauzo ya silaha na kutoa mafunzo ya kijeshi kwa makundi ya wabeba silaha katika nchi za Kiafrika ambazo zinakabiliwa na migogoro ya ndani, mauaji na uvamizi.” Katika uwanja huo tunaweza kushuhudia kuhusika moja kwa moja utawala huo katili katika mapigano yanayoendelea nchini Nigeria, mashinikizo na ukatili dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo, mapigano nchini Cameroon, njama za kuigawa Sudan zilizopelekea  kujitenga Sudan Kusini na kadhalika ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme la al-Nahdha katika mpaka wa Ethiopia, Misri na Sudan. Sheikh Adam Suhu, mjumbe wa Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria anasema: “Serikali ya Nigeria chini ya upenyaji wa kisiasa wa utawala wa kifalme wa Saudia, Marekani na utawala wa Kizayuni, inatekeleza njama pamoja na tawala hizo dhidi ya Waislamu wa Kishia wa nchi hiyo.” Mwisho wa kunukuu. Ukweli ni kwamba, kujiri mabadiliko ya kisiasa na matukio ya eneo la Mashariki ya Kati na kadhalika hatua ya baadhi ya nchi za Kiarabu ya kujikurubisha kwa utawala huo khabithi, kumeufanya uongeze juhudi zake za kujitanua na kupenya katika nchi za bara la Afrika. Naye Hisham al-Haji, mwandishi wa habari na mbunge wa zamani katika bunge la Tunisia anasema: “Utawala wa Kizayuni unajipenyeza barani Afrika na umeandaa siasa maalumu kwa ajili ya kufikia malengo yake machafu.” Mwisho wa kunukuu. Hatua hizo za utawala wa Kizayuni zinatekelezwa katika hali ambayo akthari ya viongozi wa nchi za Kiafrika wakiwemo wa Afrika Kusini wamekuwa na misimamo mikali kuhusiana na siasa za uvamizi na ubaguzi za Israe. Baadhi ya viongozi wa Afrika sambamba na kusisitiza kwamba matatizo mengi ya bara hilo yanatokana na uingiliaji na siasa chafu za madola ya kigeni ukiwemo utawala haramu wa Kizayuni, wanaamini kwamba mataifa ya bara hilo yanatakiwa kuwa macho dhidi ya siasa hizo.

Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel na mtenda jinai mkuu

Katika uwanja huo inaonekana kwamba, kuchukuliwa stratijia maalumu na nchi za bara la Afrika na kadhalika Umoja wa Afrika kuhusiana na siasa za kupenda kujitanua za Israel, kunaweza kufanikisha kuzuiwa malengo machafu ya utawala huo wa Kizayuni barani humo. Indhari ya Ali al-Haj, Katibu Mkuu wa Chama cha Kongresi ya Kitaifa nchini Sudan imetolewa katika mtazamo huo.