Mkutano wa Kimataifa wa Quds wafanyika nchini Morocco
Mkutano wa Tano wa Kimataifa kuhusu Quds umefanyika mjini Rabat, Morocco na kuhudhuriwa na wataalamu kadhaa wa kimataifa.
Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki Zisizoweza Kuporwa za Taifa la Palestina ndiyo iliyoitisha mkutano huo wa kimataifa na kuhudhuriwa na wataalamu kadhaa akiwemo Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya kisiasa na Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Kiislamu OIC.
Mkutano huo wa Rabat ambao umebeba kaulimbiu isemayo: "Palestina miaka 50 baada ya kukaliwa kwa mabavu na miaka 25 baada ya makubaliano ya Oslo" ulianza jana na utadumu kwa muda wa siku mbili.
Waitishaji wa mkutano huo wanasema kuwa, mkutano huo ni fursa nzuri ya kubadilishana mawazo kuhusu Quds hasa kutokana na matukio ya hivi karibuni yaliyoukumba mji mtakatifu wa Quds.
Cha kusikitisha ni kuwa mmoja wa Wazayuni makatili na mtenda jinai ameshiriki kwenye mkutano huo na suala hilo limewakasirishwa wakazi wa Rabat ambao wamekusanyika mbele ya Bunge la nchi yao Morocco wakilaani kualikwa mtenda jinai hiyo katika mkutano huo wa kimataifa.