Makumi ya wahanga wa magendo ya binadamu wakombolewa Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i46818-makumi_ya_wahanga_wa_magendo_ya_binadamu_wakombolewa_sudan
Maafisa wa serikali ya Sudan wametangaza kuwa, wahanga wapatao 139 wa magendo ya binadamu waliokuwa wakishikiliwa mateka wamekombolewa kutoka mikononi mwa magenge ya magendo ya binadamu mashariki mwa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 16, 2018 08:23 UTC
  • Makumi ya wahanga wa magendo ya binadamu wakombolewa Sudan

Maafisa wa serikali ya Sudan wametangaza kuwa, wahanga wapatao 139 wa magendo ya binadamu waliokuwa wakishikiliwa mateka wamekombolewa kutoka mikononi mwa magenge ya magendo ya binadamu mashariki mwa nchi hiyo.

Gavana wa jimbo la Kassala la mashariki mwa Sudan, Adam Jama’a, ameziambia duru za habari kwamba, askari usalama wa nchi hiyo wamefanikiwa kuwakomboa mateka 139 waliokuwa wakishikiliwa na magenge yanayojishughulisha na magendo ya binadamu.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, askari usalama wa Sudan wamefanikiwa pia kuwatia mbaroni wanachama kadhaa wa magenge yanayojishughulisha na biashara haramu ya magendo ya binadamu.

Gavana wa jimbo la Kassala amezitaka taasisi za kimataifa ambazo ni amilifu katika kupambana na magendo ya binadamu kuisaidia Sudan katika kupambana na biashara hiyo haramu.

Kampeni ya kupambana na magendo ya binadamu

Adam Jama'a pia ameeleza kuwa, kuna haja kwa Sudan kusaidiwa katika vita dhidi ya magendo ya buinadamu kwa sababu kuna wanawake na watoto wengi ambao wamo katika hatari ya kutekwa nyara na magenge ya wahalifu wa magendo ya binadamu.

Bunge la Sudan mwanazoni mwa mwaka jana lilipasisha sheria ya kupambana na magendo ya binadamu ambapo watu wanaojihusisha na biashara hiyo watakabiliwa na adhabu ya kunyongwa au kifungo cha kuanzia miaka mitano hadi 20. 

Hata hivyo licha ya kupita zaidi ya mwaka tangu sheria hiyo ipasishwe hadi sasa haijatekelezwa kivitendo na  matukio ya magendo ya binadamu yanaendelea kuripotiwa nchini Sudan.