Uchunguzi kuhusu mauaji ya wanahabari Warussia nchini CAR
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i47214-uchunguzi_kuhusu_mauaji_ya_wanahabari_warussia_nchini_car
Uchunguzi umeanzishwa kuhusu mauaji ya waandishi wa habari watatu raia wa Russia ambao walikwenda Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) kuchunguza suala la kuwepo kitengo cha askari mamluki wa Wagner.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 03, 2018 20:56 UTC
  • Uchunguzi kuhusu mauaji ya wanahabari Warussia nchini CAR

Uchunguzi umeanzishwa kuhusu mauaji ya waandishi wa habari watatu raia wa Russia ambao walikwenda Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) kuchunguza suala la kuwepo kitengo cha askari mamluki wa Wagner.

Serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati imeanzisha uchunguzi ili kujua sababu za mauaji ya waandishi hao wa habari. Uchunguzi huo unasimamiwa na Wizara ya Sheria, kupitia Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Bangui. Uchunguzi huu unaendeshwa na polisi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa msaada wa polisi wa Umoja wa Mataifa.

Tayari mauaji ya waandishi hao wa habari yameibua suala la kuzorota kwa usalama nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati. Mauaji haya yanahusiana na kutolewa kwa ripoti ya jopo la wataalamu wa Umoja wa Mataifa.

Mwezi uliopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa mara nyingine lilitoa wito wa kusitishwa mapigano ya ndani katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Taarifa iliyotolewa na Baraza la Usalama ilielezea wasiwasi wa wanachama wa baraza hilo kuhusu mashambulizi yanayoendelea kufanywa na makundi ya waasi katika mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Bangui na maeneo mengine ya nchi hiyo na kutangaza kuwa, inalaani mashambulizi yote yanayofanywa dhidi ya raia, askari wa kulinda amani na wanaharakati wa kutetea haki za binadamu ambayo yanaua na kujeruhi idadi kubwa ya watu.

Wanamgambo Wakristo wa Anti-Balaka  huko Jamhuri ya Afrika ya Kati

Machafuko nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati yaliibuka mwaka 2013, baada ya waasi wa Seleka kumuondoka madarakani aliyekuwa rais wa taifa hilo, François Bozizé, huku mgogoro ukishadidi zaidi baada ya waasi wa Kikristo wenye kufurutu ada wa Anti-Balaka kuanzisha mauaji ya kutisha dhidi ya jamii ya Waislamu, ambapo maelfu ya watu waliuawa na wengine wengi kuwa wakimbizi. Hivi sasa kuna askari 10,000 wa kulinda amani katika nchi hiyo iliyo katikati mwa bara la Afrika lakini hawajaweza kutuliza hali ya mambo na mapigano ya hapa na pale yangali yanaendelea.