Wahajiri wanne wapoteza maisha baada ya boti kuwaka moto Tunisia
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tunisia imetangaza habari ya kupoteza maisha wahajiri wanne baada ya boti yao kuungua moto katika fukwe za Sfax, mashariki mwa nchi hiyo.
Taarifa ya wizara hiyo imesema kuwa, wapiga mbizi kutoka jeshi la majini la nchi hiyo, jana waliopoa viwiliwili vinne vya wahajiri wa Kiafrika akiwemo raia mmoja wa Tunisia katika fukwe za Sfax.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, askari wa kulinda mipaka wa Tunisia wamefanikiwa kuokoa wahajiri 14 wakiwemo raia wanane wa Ivory Coast, wawili wa Congo na wanawake wanne, ingawa haikutajwa wanawake hao wanne ni raia wa wapi.

Kwa mujibu wa wizara hiyo ya mambo ya ndani ya Tunisia, ajali hiyo ilitokea juzi Ijumaa wakati maafisa wa gadi ya ufukweni ya Tunisia ilipoiona boti hiyo ikisafiri kimagendo na wakatoa onyo isimame, lakini boti hiyo haikusimama.
Baada ya hapo maafisa hao waliitupia boti hiyo mabomu ya chupa (Molotov Cocktail) na kusababisha kuungua sehemu moja ya boti hiyo.
Itakumbukwa kuwa mwezi Juni mwaka huu pia, wahajiri 80 walikufa maji baada ya boti yao kuzama katika fukwe za Tunisia.