Serikali ya Sudan yavunjwa kwa mgogoro wa kiuchumi
-
Rais wa Sudan, Field Marshal Omar Hassan al Bashir
Rais Omar al Bashir wa Sudan ameivunja serikali ya nchi hiyo na kuteua waziri mkuu mpya katika hatua inayoonekana ni ya kukabiliana na mgogoro wa kiuchumi wa nchi hiyo.
Jana al Bashir alimteua Moataz Moussa kuwa waziri mkuu mpya wa Sudan kushika nafasi ya Bakri Hassan Saleh. Kabla ya hapo Moataz Moussa alikuwa waziri wa vyanzo vya maji, kilimo cha umwagiliaji na umeme. Saleh ambaye alikuwa anatumikia vyeo viwili vya waziri mkuu na makamu wa rais, alipewa nafasi ya uwaziri mkuu na al Bashir mwaka 2017 na hivi sasa atabakia na cheo kimoja cha makamu wa rais.
Waziri Mkuu mpya anatarajiwa kuunda serikali itakayokuwa na mawaziri 21 kutoka 31 wa serikali ya hivi sasa, suala ambalo linaonekana wazi kuwa linalenga kupunguza matumizi ya serikali. Taarifa iliyotolewa na ofisi ya rais wa Sudan imesema kuwa, hatua hiyo imebidi kuchukuliwa ili kukabiliana na changamoto za kiuchumi zinazoikabili nchi hiyo ya katikati mwa Afrika. Katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni, wananchi wa Sudan wamekuwa wakiteseka kwa upungufu wa vitu vingi kama vile mikate, mafuta na sarafu inayoyumba. Thamani ya dola ya Marekani imepanda katika miezi ya hivi karibuni kutoka pauni 30 za Sudan kwa kila dola moja hadi kufikia pauni 47 katika soko lisilo rasmi.
Serikali ya Rais Omar al Bashir wa Sudan imelegeza kamba sana katika misimamo yake na kujikurubisha kwa Marekani na vibaraka wake hasa Saudi Arabia kiasi cha kuingia vitani kufanya jinai dhidi ya Waislamu wa Yemen. Kubadilika huko kwa siasa za serikali ya Sudan kumepelekea kuondolewa vikwazo vya miaka 20 vya Marekani dhidi ya Khartoum mwaka jana. Viongozi wa Sudan walikuwa na tamaa kuwa, kuondolewa vikwazo hivyo kutaondoa matatizo yao ya kiuchumi, lakini hali imekuwa mbaya zaidi na soko lisilo rasmi la mauzo ya dola ya Kimarekani limehodhi mfumo wa kawaida wa kibenki wa nchi hiyo.