Benki ya Maendeleo ya Afrika yaipa Senegal msaada wa dola milioni 200
Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imeipa Senegal msaada wa zaidi ya dola milioni mia mbili za Kimarekani.
Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa Jumanne mjini Dakar kati ya Benki ya AfDB na Senegal, pande hizo mbili zimetiliana saini mikataba minne ya kuisaidia kifedha Senegal, yenye thamani ya karibu dola milioni 211 za Kimarekani.
Makubaliano ya kwanza yanahusiana na kukarabatiwa barabara kusini mwa Senegal na ya pili ni kuhusu kukwamua maeneo yaliyokwama ya uzalishaji bidhaa.

Makubaliano ya tatu baina ya pande hizo mbili yanahusiana na mradi wa maendeleo ya vijana huku makubaliano ya nne na ya mwisho yakihusiana na mradi wa kusaidia mpango wa dharura wa ustawi wa jamii.
Hii ni katika hali ambayo mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu, Benki ya Maendeleo ya Afrika AfDB na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO zilikubaliana kuendeleza juhudi za pamoja za kuongeza uwekezaji katika sekta ya kilimo barani Afrika ili kukomesha njaa na utapiamlo kwa lengo la kupanua wigo wa ustawi na maendeleo barani humo.
Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Jose Graziano da Silva, alisema kuwa , FAO na Benki ya Maendeleo ya Afrika zimeamua kupanua wigo wa ushirika baina yao ili kuweza kusaidia mataifa ya Afrika kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu SDG’s, na kufadhili kilimo pamoja na sekta binafsi ambazo ndio ufunguo wa kuwatoa mamilioni ya watu katika njaa na umasikini uliokithiri barani Afrika lakini pia kuhakikisha kunakuwepo chakula cha kutosha barani humo.